Olmert: Adui yetu ni Netanyahu, si Iran, Hizbullah wala Hamas!
(last modified Wed, 30 Oct 2024 08:13:10 GMT )
Oct 30, 2024 08:13 UTC
  • Olmert: Adui yetu ni Netanyahu, si Iran, Hizbullah wala Hamas!

Waziri Mkuu wa zamani wa Israel, Ehud Olmart amesema adui wa utawala huo sio Iran, Hizbullah wala Hamas bali ni Waisraeli wenye itiikadi kali akiwemo waziri mkuu wa sasa wa utawala huo, Benjamin Netanyahu.

Olmart amesema katika mahojiano yake na televisheni ya CNN ya Marekani kwamba "Tunasikitika kwamba Netanyahu anategemea watu wenye itikadi kali na kufumbia macho vitendo vyao visivyokubalika." 

Mwezi Mei mwaka jana, Olmert alitoa wito kwa Waisraeli kumiminika mitaani kwa mamilioni na kuzingira kundi la Netanyahu, Ben Gvir na Smotrich, ambalo alisema linakanyaga sheria na kuielekeza Israel kuzimu.

Olmert amesisitiza kwamba Netanyahu anaishi ndani ya mapovu ambako amejitenga na ukweli, huku akijigamba kuwa yeye na wenzake ndani ya mapofu hayo wanapigana kwa ajili ya uwepo wa Israel!

Septemba mwaka jana waziri mkuu huyo wa zamani wa Israel alizusha mjadala mkubwa kuhusu mustakbali wa utawala ghasibu wa Israel pale alipotahadharisha juu ya uwezekano wa kutokea vita vya ndani baina ya Wayahudi wanaoshikamana na dini ya mahasimu wao.