Sheikh Qassem: Hizbullah itazima 'mpango mkubwa' wa Israel katika eneo
(last modified Thu, 31 Oct 2024 02:37:05 GMT )
Oct 31, 2024 02:37 UTC
  • Sheikh Qassem: Hizbullah itazima 'mpango mkubwa' wa Israel katika eneo

Katibu Mkuu mpya wa Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon amesema kundi hilo la mapambano ya Kiislamu litaendelea kupambana kwa shabaha ya kusambaratisha njama za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya eneo zima la Asia Magharibi.

Sheikh Naim Qassem ameonya kwamba, utawala haramu wa Israel na waungaji mkono wake wa Magharibi na Ulaya wanashirikiana katika "mpango mkubwa" wa kulitawala eneo hili.

Aliwaambia hadhira katika hotuba yake ya kwanza ya televisheni jana Jumatano baada ya kuteuliwa kwamba, mpango wake wa kivitendo ni kuendeleza njia na kazi ya mtangulizi wake, Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah. Sheikh Qassem amebainisha kuwa, "Tutaendelea kutekeleza mpango wa vita uliowekwa na Sayyid Nasrullah, na tutabaki kwenye njia ya vita ndani ya mwelekeo wa kisiasa uliowekwa."

Katibu Mkuu wa Hizbullah amesisitiza kuwa, kuiunga mkono Gaza ni muhimu ili kukabiliana na hatari inayoletwa na utawala wa Kizayuni kwa eneo zima.

Wanamuqawama wa Hizbullah ya Lebanon

Kadhalika Sheikh Qassem amesisitiza kuwa, utawala ghasibu wa Israel haujawahi kufuata sheria za kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa.

"Israel haijawahi kufungamana na Azimio Nambari 1701, na imekiuka mamlaka ya anga na bahari ya Lebanon mara 39,000," alisema, akiashiria azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililomaliza vita vya 2006, na kutaka kuheshimiwa uhuru na mamlaka ya kuhjitawala Lebanon

Kiongozi huyo wa Hizbullah ameeleza bayana kuwa, ni Muqawama na wala sio maazimio ya kimataifa, ambao ulivifurusha vikosi vya Israeli kutoka Lebanon mwaka 2000.

Tags