WHO: Hali ya watoto katika Ukanda wa Gaza ni mbaya
(last modified Sun, 03 Nov 2024 12:50:49 GMT )
Nov 03, 2024 12:50 UTC
  • WHO: Hali ya watoto katika Ukanda wa Gaza ni mbaya

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ametahadharisha kuhusu hali mbaya ya watoto wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza kufuatia kuendelea mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ameandika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa "X" kwamba, kwa akali watoto wanne walijeruhiwa katika shambulio la anga la Israel dhidi ya kituo cha afya katika Ukanda wa Gaza.

Adhanom Ghebreyesus ameongeza kuwa shambulio hilo dhidi ya kituo cha afya katika Ukanda wa Gaza lilifanyika katika eneo ambalo liliafikiwa "kusitishwa kwa mapigano ili kuendelea kutoa chanjo."

Wakati huo huo, Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) pia umetahadharisha kuwa, uamuzi wa utawala wa Israel wa kupiga marufuku Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi wa Palestina, UNRWA unaweza kusababisha vifo vya watoto zaidi, jambo ambalo ni aina ya adhabu ya pamoja kwa wananchi wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.

Kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele ndivyo hali ya usalama na kibinadamu huko Ukanda wa Gaza inavyozidi kuzorota huku raia na hata wafanyakazi wa kutoa misaada wakisalia wakikabiliwa na hali ngumu.