Radiamali ya UN kwa vitendo vya kichokozi na kujitanua vya Israel
Umoja wa Mataifa na viongozi wa Palestina wamelaani vikali mipango ya Israel ya kupanua ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu.
Kuhusiana na suala hilo Nicolay Mladenov Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na Mchakato wa Amani ya Mashariki ya Kati Jumatatu wiki hii alilaani hatua ya utawala wa Kizayuni ya kupanua ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina.
Wakati huo huo Saib Uraiqat Katibu Mkuu wa Kamati ya Utekelezaji ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina ametangaza kuwa hatua hizo za utawala wa Kizayuni zinaonyesha namna jamii ya kimataifa ilivyoshindwa kusitisha ujenzi wa vitongoji unaofanywa na Israel.
Masisitizo ya kimataifa kwamba ujenzi wa vitongoji unaofanywa na utawala ghasibu wa Kizayuni katika maeneo malimbali ya Palestina ni kinyume cha sheria; na kwamba hatua zinazotekelezwa na utawala huo zinakwamisha mchakato wa amani, yote hayo yamewadhihirishia zaidi walimwengu kuhusu sura halisi ya utawala huo ya kupinga amani na namna Israel inavyopuuza sheria za kimataifa.
Imeelezwa kuwa waungaji mkono wa utawala wa Kizayuni hivi sasa wanajaribu kuuonyesha utawala wa Kizayuni kuwa ni utawala eti unaopenda amani katika fremu ya mchakato wa kusaka amani sambamba na kuanza kutekelezwa duru mpya ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni ambayo inaambatana na kushadidi hatua za uharibifu na kupenda kujitanua za utawala huo.
Hii ni katika hali ambayo kupenda kujitanua na uvamizi wa mara kwa mara wa Israel katika ardhi za raia wa Palestina ni moja ya misingi ya utawala huo unaoikalia Quds kwa mabavu huku vyama na makundi yote ndani ya utawala wa Kizayuni yakielekeza harakati zao katika mkondo huo. Utawala wa Kizayuni unatekeleza vitendo vyake vya kujitanua katika maeneo ya Palestina; ambapo kwa mujibu wa maazimio ya kimataifa kama lile la Geneva, utawala huo hauruhusiwi kutekeleza hatua yoyote ya kughusubu na kuvamia maeneo ya Palestina.
Hii ni katika hali ambayo maazimio ya Umoja wa Mataifa pia yanalaani vitendo vya kichokozi vya utawala wa Kizayuni vya kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na kutaka kubomolewa vitongojii hivyo.
katika mazingira kama hayo sisitizo la utawala wa Kizayuni la kuendeleza siasa zake za kupenda kujitanua zimekabiliwa na radiamali kubwa kimataifa na malalamiko ya Wapalestina. Utawala wa Kizayuni hata hivyo sambamba na kupanua ujenzi huo katika maeneo ya Palestina, unaendesha pia mazoezi ya kijeshi katika ardhi inazozikalia kwa mabavu lengo likiwa ni kuzusha hofu na wahka miongoni mwa raia wa Kipalestina ili kuzidi kuwakandamiza.
Katika fremu hiyo jeshi la utawala wa Kizayuni tangu Jumatatu wiki hii limeanzisha duru yake ya maneva ya kijeshi yatakayodumu kwa siku kadhaa katika eneo la al Jalil kaskazini mwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu; hiyo ikiwa ni katika kuendelezwa vitendo vya kijuba vya Israel vya kushadidisha ukandamizaji wake dhidi ya mapambano ya Intifadha ya wananchi wa Palestina. Utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukiendesha maneva mbalimbali katika maeneo ya Palestina unayoyakalia kwa mabavu ikiwa ni katika kuendeleza siasa zake za kupenda vita katika eneo, kuwakandamiza na kuwaua raia wa Palestina wasio na hatia.