Kuendelea misaada ya silaha ya Marekani kwa Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i121058-kuendelea_misaada_ya_silaha_ya_marekani_kwa_israel
Jinai za Israel dhidi ya Wapalestina wanaoishi Gaza zinaendelea kwa kuungwa mkono wa nchi za Magharibi hususan Marekani.
(last modified 2025-01-05T23:32:34+00:00 )
Jan 05, 2025 23:32 UTC
  • Kuendelea misaada ya silaha ya Marekani kwa Israel

Jinai za Israel dhidi ya Wapalestina wanaoishi Gaza zinaendelea kwa kuungwa mkono wa nchi za Magharibi hususan Marekani.

Kuhusiana na hilo, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani imeripoti kuwa, imeliarifu Bunge la nchi hiyo Congress kwa njia isiyo rasmi kuhusu uwezekano wa kuuzwa shehena kubwa ya silaha kwa utawala wa Kizayuni yenye thamani ya dola bilioni 8, zikiwemo ndege za kivita na helikopta.

Tovuti ya habari ya Marekani Axios ilinukuu vyanzo viwili visivyojulikana vilivyo na taarifa za moja kwa moja kuhusu suala hilo ikisema kwamba, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani ilikuwa imearifu Bunge la Kongresi "kwa njia isiyo rasmi" kuhusu mpango wa silaha za dola bilioni 8 kwa Israel.

Kifurushi hicho cha silaha kinajumuisha makombora yanayotumiwa na ndege za kivita na helikopta za mashambulizi pamoja na mizinga na aina kadhaa za mabomu.

Mpango huo, ambao huenda ukawa mauzo ya mwisho ya silaha ambayo Joe Biden ataidhinisha kwa Israel, unakuja miezi michache baada ya utawala wake kuidhinisha mauzo ya dola bilioni 20 ya ndege za kivita na vifaa vingine vya kijeshi kwa utawala huo licha ya matakwa ya kimataifa ya kutaka kuwepo marufuku ya silaha dhidi ya Tel Aviv kutokana na  vita vyake vya miezi 15 huko Gaza.

Biden anatarajiwa kuondoka Ikulu mnamo Januari 20, huku Rais mteule wa Republican Donald Trump akimrithi ili kuendeleza sera za Marekani zinazounga mkono Israel na kuchochea mashine ya vita ya utawala huo katili na wa kibaguzi.

Marekani imeendelea kuipatia silaha Israel licha ya walimwengu kulalamimikia hilo

 

Ola Awad, Mkuu wa Ofisi Kuu ya Takwimu ya Palestina alitangaza kupungua kwa 6% ya idadi ya watu wa Gaza kutokana na mauaji ya kimbari ya Israel na kusema: "Idadi ya watu wa Gaza imepungua kwa watu 160,000 ikilinganishwa na mwaka jana na imefikia watu 2,100,000." Ameongeza kuwa: Zaidi ya watu 45,500 wameuawa shahidi katika mashambulizi ya utawala wa Kizayuni tangu tarehe 7 Oktoba 2023; Wapalestina 100,000 walikimbia makazi yao, zaidi ya watu 108,000 walijeruhiwa na takriban watu 11,000 hawajulikani walipo, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Kimsingi ni kuwa, katika miezi ya hivi karibuni, licha ya kushadidi jinai za Israel dhidi ya wakaazi wa Gaza, lakini nchi za Magharibi zinaendelea kuipa Israel silaha. Licha ya madai yao yote ya demokrasia na kuheshimu matakwa ya raia wao, lakini zimejifanya vipofu na kutia pamba masikioni na hivyo kujifanya kuwa hazikisii kilio cha walimwengu kuhusiana na jinai za Israel.

Karibu Wapalestina 46,000 wameuawa shahidi tangu kuanza mauaji ya kimbari ya Israel katika Ukanda wa Gaza Oktoba 2023.

 

Ijapokuwa Rais mteule wa Marekani Donald Trump ametangaza na kusisitiza juu ya Washington kuendelea kuiunga mkono na kuisaidia Israel, lakini Rais Joe Biden wa Marekani pia ameafiki mpango wa kupelekewa Israel silaha zenye thamani ya dola bilioni 8 katika wiki za mwisho za utawala wake na hivyo kuiruhusu  Israel iendelee kufanya mauaji dhidi ya Wananchi madhlumu wa Palestina.

Kwa upande mmoja, Marekani na washirika wake wanasafirisha silaha na zana za kijeshi kwa Israel, na kwa upande mwingine, wanazuia juhudi za kuendelezwa mazungumzo na kufikiwa usitishaji vita, na wakati huo huo, Israel inaendeleza jinai zake dhidi ya Wapalestina.

Pamoja na hayo, baada ya zaidi ya siku 450 kupita tangu kuanza jinai za Israel; vyombo vya habari vya Kizayuni vimekiri juu ya kushindwa kwa utawala huo kufikia malengo yaliyowekwa kwa ajili ya vita hivi na vimetangaza kwamba: Operesheni ya mashambulio huko Gaza haijafikia malengo yoyote ya kistratijia ya vita yaliyoainishwa na utawala huo.