Mpango wa Trump kwa ajili ya Gaza; njama za kuifuta Palestina
Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria upinzani mkubwa wa nchi za eneo na kimataifa dhidi ya mpango haramu wa Rais wa Marekani kuhusu Gaza na kueleza kwamba, mpango huo wa kuwahamisha kwa nguvu watu wa Palestina kutoka Gaza kwa mujibu wa mpango wa kikoloni wa "kuifuta Palestina".
Araghchi sambamba na kulaani njama hiyo hatari ametoa mwito wa kuweko msimamo mmoja wa jamii ya kimataifa na nchi za Kiislamu mkabala wa njama hiyo hatari.
Rais wa Marekani Donald Trump hivi karibuni alitoa kauli zenye utata akitaka kuhamishwa kikamilifu Wapalestina kutoka katika Ukanda wa Gaza na kuwapa makazi mengine katika nchi jirani za Kiarabu. Trump alidai kuwa watu wa Gaza wanatazamia kuondoka katika eneo hili iwapo kutakuweko mahala pengine panapofaa kwa ajili yao, na kwa maoni yake, kuna nchi zinazoweza kuandaa hilo.
Mpango huu umekabiliwa na majibu hasi ya kikanda na kimataifa. Jambo muhimu ni kwamba hata washirika wa Magharibi wa Marekani kama Ujerumani na Ufaransa, zimelaani mpango huu. Wakosoaji wa mpango huu wanasema kuwa, hatua hiyo ni ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu na njama za kufuta kaumu na kizazi katika Ukanda wa Gaza.
Katika taarifa isiyo na mfano wake na ya ghafla, Rais wa Marekani alisema hivi karibuni mbele ya Waziri Mkuu wa Israel huko White House kwamba, Marekani inakusudia kuutwaa Ukanda wa Gaza na pia kuwa kuna uwezekano wa nchi hiyo kutambua rasmi udhibiti wa utawala wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Awali, Trump alisema kuwa Wapalestina wanaoishi Gaza wanapaswa kuhamishiwa Misri na Jordan ili Gaza iweze kujengwa upya. Sasa Rais huyo mwenye matamshi mengi ya utata ameenda mbali zaidi na kuzungumzia unyakuzi wa kipande hiki kidogo cha ardhi lakini chenye watu wengi zaidi duniani kilichoko kwenye ufuo wa mashariki wa Bahari ya Mediterania.
Jumapili iliyopita, Rais wa Marekani Donald Trump alikariri tena bila ya aibu kutoa pendekezo lake tata la kulinyakua na kulidhibiti eneo la Ukanda wa Ghaza, akisema amejitolea "kulinunua na kulimiliki" eneo hilo lililoharibiwa na vita.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ndege ya Air Force One siku ya Jumapili, Trump alisema Ghaza inapasa izingatiwe kama "eneo kubwa la mali isiyohamishika" na kwamba nchi zingine za Mashariki ya Kati zinaweza kuwa na jukumu la kushughulikia ujenzi wake mpya.
“Kama sisi tunavyoijenga upya, tunaweza kuipa mataifa mengine pia katika Mashariki ya Kati kujenga baadhi ya sehemu zake; watu wengine wanaweza kufanya kazi hiyo, kupitia mwamko wetu”, ametamka rais huyo wa Marekani, huku akisisitiza kwa kusema: "lakini tumejitolea kuimiliki, kuichukua, na kuhakikisha kuwa Hamas hairudi tena. Hakuna kitu cha kukirudia tena. Ni eneo lililobomolewa."
Trump amedai pia kuwa Wapalestina waliolazimika kuyahama makazi yao wangependelea wasirudi tena Ghaza licha ya pendekezo lake kukabiliwa na upinzani mkali wa wawakilishi wa Palestina na sehemu kubwa ya jamii ya Kimataifa.
Mpango huo wa Trump umeendelea kulaaniwa kila pembe ya dunia. Hata hivyo Trump akiwa na nia ya kufikia lengo lake ameanza kutoa vitisho dhidi ya mataifa kama Misri na Jordan ambayo kimsingi anayataka yawapokee Wapalestina watakaohamishwa kutoka Gaza.
Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa, anaweza akafikiria kusitisha msaada kwa Jordan na Misri ikiwa zitakataa kuwapokea Wapalestina, baada ya kutekeleza mpango wake wa kuwahamaisha kwa nguvu wananchi hao katika ardhi yao ya Ukanda wa Ghaza ili kulihodhi na kulimiliki eneo hilo lililowekewa mzingiro.

Mfalme Abdullah II wa Jordan ambaye nchi yake hadi mwaka 2023 ilikuwa ya nne duniani inayopokea msaada mkubwa kutoka Marekani wa dola bilioni 1.72, jana Jumanne aliwasili huko Washington Marekani ili kukutana na kuzungumza na Trump.
Mapema juzi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa wa Misri, Badr Abdelatty, alimueleza mwenzake wa Marekani Marco Rubio kwamba, mataifa ya Kiarabu yanaunga mkono msimamo wa Wapalestina wa kukataa mpango wa Trump wa kuwahamisha Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza na kulikalia kwa mabavu eneo hilo.
Tishio la Trump cha kusitisha misaada kwa Misri na Jordan kimetolewa sambamba na kutishia pia kuwa atayafuta makubaliano ya kusitisha vita dhidi ya Ukanda wa Gaza ikiwa mateka wote wa Kizayuni hawataachiliwa ifikapo Jumamosi baada ya Harakati ya Hamas kutangaza kuwa inasimamisha mchakato huo kutokana na Israel kukiuka makubaliano ya kusitisha vita.
Licha ya vitisho hivyo, viongozi wa Misri na Jordan wanafahamu vyema ukweli huu kwamba, kuukubali mpango wa Trump kuhusu Gaza na kuafiki kuwahamishwa wakaazi wa eneo hilo hadi katika nchi hizi mbili hakutakuwa na maana nyingine ghairi ya kuisaliti kadhia ya Palestina.
Aidha hatua hiyo itasababisha matatizo makubwa kwa Misri na Jordan. Kadhalika wananchi wa Gaza ambao wamesimama kidete kukabiliana na mashambulizi makali ya utawala wa Kizayuni kwa zaidi ya miezi 15 na hawako tayari kuondoka Gaza, kamwe hawatakuwa tayari kuondoka katika ardhi yao hata kwa kulazimishwa na kutumiwa nguvu na mabavu dhidi yao.