Kukimbia wanajeshi wa Marekani San'a ni ushindi mkubwa kwa Yemen
-
Sayyid Abdul Malik al-Houthi
Kiongozi wa harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema kuwa, kukimbia wanajeshi wanamaji wa Marekani mjini San'a ni ushindi mkubwa kwa wananchi wa Yemen na kusisitiza kuwa, kukimbia wanajeshi hao vamizi wa Marekani ni ishara ya kushindwa mradi wa kupenda kujitanua Washington nchini Yemen.
Sayyid Abdul Malik al-Houthi amesema hayo katika hotuba aliyotoa jana (Jumanne) jioni na kutilia mkazo suala hilo akisema: Kwa baraka ya Mwenyezi Mungu, wananchi wa Yemen wamepata ushindi mkubwa.
Amesisitiza kuwa, mataifa ya dunia hayawezi kupata uhuru wa kweli na kuishi kibinadamu na kwa heshima kama walivyokadiriwa na Muumba, madhali wako chini ya udhibiti wa Marekani.
Amesisitiza mara kadhaa kwamba kukimbia wanajeshi wanamaji wa Marekani huko San'a, mji mkuu wa Yemen ni kufeli mradi wa Marekani wa kutaka kuitawala na kuidhibiti Yemen na kwamba hayo ni matunda ya mapinduzi ya Septemba 21 ya wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu.
Vilevile amesema: "Maadamu Marekani inatawala masuala ya nchi, nchi hiyo haiwezi kuwa huru na kujikomboa kutoka kwenye makucha ya ubeberu wa Marekani kunawadhaminia watu, heshima, ubinadamu na uhuru wao na hayo ndiyo matunda wanayojifakharisha nayo wananchi wa Yemen hivi sasa baada ya kuwatimua Wamarekani.
Tangazo la Kiongozi wa Ansarullah ya Yemen kuhusu kushindwa mradi wa Marekani wa kuidhibiti nchini hiyo limekuja baada ya miezi kadhaa ya matamshi ya Waziri Mkuu wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen, Abdulaziz bin Habtour ambaye mwezi Mei uliopita alitahadharisha kuhusu mradi wa kinyama unaoendelezwa na baadhi ya nchi za Magharibi na utawala haramu wa Israel zikiongozwa na Marekani unaolenga kuvuruga mshikamano, umoja wa ardhi ya Yemen na kuigawa vipande vipande nchi hiyo ngangari ya Kiislamu.