Utawala wa Kizayuni; muuaji wa 70% ya waandishi wa habari duniani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i122744-utawala_wa_kizayuni_muuaji_wa_70_ya_waandishi_wa_habari_duniani
Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari nchini Marekani sambamba na kutangaza kuwa, idadi kubwa ya waandishi wa habari waliuawa duniani kote mwaka jana imeeleza kwamba, utawala wa Kizayuni umehusika na mauaji ya takriban asilimia 70 ya waandishi hao.
(last modified 2025-02-14T23:11:35+00:00 )
Feb 14, 2025 23:11 UTC
  • Utawala wa Kizayuni; muuaji wa 70% ya waandishi wa habari duniani

Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari nchini Marekani sambamba na kutangaza kuwa, idadi kubwa ya waandishi wa habari waliuawa duniani kote mwaka jana imeeleza kwamba, utawala wa Kizayuni umehusika na mauaji ya takriban asilimia 70 ya waandishi hao.

Waandishi wa habari ni miongoni mwa wahanga wakuu wa mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni huko Gaza. Jinai iliyofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika vita vya miezi 15 dhidi ya Gaza haikuwa na mfano wake katika vita vya miongo ya hivi karibuni.

Wakati wa uvamizi wa Marekani dhidi ya Vietnam, ambao ulidumu karibu miaka 20, waandishi wa habari 63 waliuawa, na waandishi wa habari 17 waliuawa katika Vita vya Peninsula ya Korea katika vilivyodumu kwa muda wa miaka 3.

Hii ni katika hali ambayo, Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari imetangaza kuwa, operesheni ya kijeshi ya Wazayuni dhidi ya Wapalestina huko Gaza imesababisha kuuawa shahidi waandishi wa habari 85 na jeshi dhalimu la Israel.

Wakati huo huo, vyanzo vya Wapalestina vimeripoti kuuawa shahidi na Israel waandishi wa habari 205 huko Gaza wakati wa vita katika eneo hilo.

Wazayuni walifanya mashambulizi 1,600 dhidi ya waandishi wa habari na hata waliharibu kanali ya televisheni ya watoto.

Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari ilitangaza kuwa, kwa akali imerekodi mauaji ya watu 10 yaliyokuwa na malengo maalumu na yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni na inachunguza mauaji mengine 20 ambayo huenda nayo yalikuwa yamepangwa na kuratibiwa.

Waandishi habari wakkiwa wamebeba maiti ya mwenzao wakienda kuzika

 

Takwimu hizi zinaonyesha kuwa, Gaza lilikuwa eneo hatari zaidi duniani mwaka jana. Waandishi wa habari waliuawa na utawala wa Kizayuni kwa sababu tu walikuwa wakitekeleza majukumu yao ya kikazi, yaani kuakisi na kuripoti habari za matukio ya vita vya Gaza.

 Katika moja ya jinai zake za kutisha, utawala wa Kizayuni uliamua kuwaua waandishi wa habari ili kuzuia kuripotiwa habari za mauaji ya halaiki huko Gaza na kwa njia hii kuzuia kuripotiwa vita vya Gaza. Lakini hatua hizo hazikuzuia kuripotiwa na kutangazwa jinai za utawala huo huko Gaza na waandishi wa habari.

Jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya waandishi wa habari na mwaka uliopita kuwa mbaya zaidi kwa waandishi wa habari kunatokea katika hali ambayo, vyombo vya habari vya Magharibi vinajaribu kuchuja habari za jinai za utawala huo ghasibu na kutoripoti kama ulivyo ukweli na uhalisia wa mambo. Kwa ujumla, hali ya waandishi wa habari huko Gaza wakiwemo waliouawa kwa sababu ya kazi zao, au waandishi wa habari na vyombo vya habari vilivyokataa kuripoti na kuakisi jinai za utawala huo, ni mambo yanayoashiria kudhoofika kwa sheria za kimataifa.

Shirin Abu Akleh, mmoja wa waandishi wa mashuhuri wa habari wa Palestina aliyeuawa kwa kupigwa risasi na jeshi la utawala haramu wa Israel

 

Jodie Ginsberg, Mkuu wa Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari, pia alitangaza kwamba hali ya waandishi wa habari huko Gaza inaonyesha kudhoofika sana kanuni na sheria za kimataifa za kuwalinda waandishi wa habari katika maeneo ya vita.

Nukta nyingine ni kwamba, utawala wa Kizayuni wa Israel unazuia uchunguzi wowote kuhusu mauaji ya waandishi wa habari huko Gaza. Kuhusiana na hilo Katibu Mkuu wa Shirikisho la Kimataifa la Waandishi wa Habari amesema, inapasa kupasisha Mkataba wa Usalama wa Wanahabari ili kukomesha mauaji ya kila mwaka ya wafanyakazi wa tasnia ya habari. Audrey Azoulay Mkurugenzi Mkuu Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) pia amesema, ni jambo lisilokubalika kwamba wanahabari wanatoa gharama ya roho na maisha yao kwa ajili ya kutekeleza jukumu lao la uanahabari. Natoa wito kwa nchi zote kusaidia wafanyakazi wa vyombo vya habari kwa mujibu wa sheria za kimataifa.