Hamas yawaachilia mateka watatu Waisraeli mkabala wa wafungwa 369 wa Kipalestina
Wanaharakati wa mapambano ya Kiislamu au Muqawama wa Gaza wamewakabidhi mateka watatu Waisraeli kwa Msalaba Mwekundu kwa kubadilishana na Wapalestina 369 ambao wataachiliwa baadaye, ikiwa ni sehemu ya mkataba wa kubadilishana mateka na wafungwa unaoendelea chini ya makubaliano ya usitishaji vita.
Wanaharakati walikuwa wamewapandisha wafungwa kwenye jukwaa huko mji wa kusini wa Gaza, Khan Yunis, ambapo Waisraeli hao walihutubia umati kabla ya kukabidhiwa kwa Msalaba Mwekundu.
Wanaume hao watatu, wakishikilia mifuko ya zawadi waliyopewa na cheti cha kuashiria mwisho wa kifungo chao, wametoa wito wa kukamilisha ubadilishanaji zaidi wa wafungwa chini ya makubaliano ya usitishaji vita. Vyanzo kutoka harakati za Hamas na Jihad Islami vimesema makundi ya muqawama yalipeleka wapiganaji wapatao 200 kwenye sherehe ya makabidhiano.
Kuachiliwa huko ni mara ya sita tangu usitishaji vita ulipoanza kutekelezwa Januari 19. Ubadilishanaji huo umetokea baada ya hofu wiki iliyopita kwamba mkataba huo ulikuwa karibu kuvunjika baada ya Israel kukataa kuruhusu msaada wa kibinadamu kuingia Gaza.
Makubaliano hayo ya usitishaji vita yamekuwa katika msukosuko mkubwa tangu Rais Donald Trump wa Marekani, alipoibua utata mkubwa na matamshi yake yaliyopendekeza kwamba Marekani inapaswa "kuichukua" Gaza, kuwahamisha watu wake, na "kumiliki" eneo hilo la Wapalestina.
Amependekeza kuwahamisha wakazi wa Gaza wapatao milioni 2.3 na kuwapeleka Misri na Jordan, akidai watafaidika zaidi.
Hamas imeuita mpango wa Trump kuwa "usio na maana na wa kijinga". Nchi za Kiarabu na Kiislamu zimepinga vikali mpango huo.
Utawala wa Kizayuni wa Israel ulilazimika kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano huko Ghaza baada ya kushindwa kufikia hata moja kati ya malengo iliyotangaza ulipoanzisha vita dhidi ya eneo hilo Oktoba 7, 2023, likiwemo la kuwakomboa mateka wake na "kuifuta" harakati ya Hamas, pamoja na kuwalazimisha wakazi wote wa Gaza walihame eneo hilo na kuelekea nchi jirani ya Misri.