Hizbullah: Kudumisha mahusiano na Iran ni kwa maslahi ya Lebanon
Mjumbe mwandamizi wa harakati ya muqawama ya Hizbullah nchini Lebanon amekosoa jinsi serikali ya Lebanon ilivyoshughulikia mgogoro wa Alhamisi katika uwanja wa ndege wa mji mkuu Beirut, akisisitiza kwamba kudumisha mahusiano yenye mlingano na Iran ni kwa maslahi ya Lebanon.
Ghaleb Abu Zeinab, mjumbe rasmi wa Ofisi ya Kisiasa ya Hizbullah, ametoa taarifa hiyo katika mahojiano na kituo cha televisheni cha al-Manar, kufuatia maandamano yenye vurugu ambayo yalizuka kwenye barabara zinazoelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Beirut-Rafic Hariri kutokana na uamuzi wa serikali ya nchi hiyo ya Kiarabu wa kupiga marufuku kwa muda ndege za Iran kutua.
Abu Zeinab amesema: "Msimamo wa serikali ya Lebanon juu ya kile kilichotokea kwenye uwanja wa ndege huko Beirut kufuatia kukataliwa kwa ndege ya Iran iliyobeba abiria wa Lebanon kutua haukuwa sahihi wala wenye matumaini."
Mkurugenzi Mkuu wa Usafiri wa Anga wa Lebanon alisema Alhamisi kuwa walikuwa wamepanga upya kwa muda baadhi ya safari za ndege ikiwa ni pamoja na kutoka Iran hadi Februari 18 kwa kuwa walikuwa wakitekeleza "hatua za ziada za usalama."
Baadaye mchana, kundi la watu wa Lebanon walifunga barabara zinazoenda uwanja wa ndege wa Beirut na kuchoma matairi ili kupinga uamuzi wa Lebanon.
Baada ya maandamano ya uwanja wa ndege, mamlaka zilisema zilikuwa zikifanya kazi kurudisha abiria wa Lebanon walioachwa Iran kwa ndege za Shirika la Ndege la Mashariki ya Kati lililoko Beirut.
Matukio hayo yalikuja sanjari na vitisho vya Israel dhidi ya ndege za Iran kutua Lebanon.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, alisema kwamba "tishio la utawala wa Kizayuni kwa ndege ya abiria iliyobeba raia wa Lebanon limevuruga safari za kawaida za ndege kwenda uwanja wa ndege wa Beirut."
Baghaei amelaani "uvunjaji mkubwa na wa mara kwa mara wa kanuni na sheria za kimataifa na ukiukaji wa mamlaka wa kitaifa wa Lebanon" unaofanywa na Israel.