Malengo maovu ya utawala wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i122784-malengo_maovu_ya_utawala_wa_kizayuni_katika_ukingo_wa_magharibi
Utawala wa Kizayuni wa Israel unaendeleza mashambulizi ya kinyama katika maeneo mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
(last modified 2025-02-15T22:51:13+00:00 )
Feb 15, 2025 22:51 UTC
  • Malengo maovu ya utawala wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi

Utawala wa Kizayuni wa Israel unaendeleza mashambulizi ya kinyama katika maeneo mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Sambamba na kusitisha vita huko Gaza, utawala ghasibu wa Israel umezidisha mashambulizi ya kijeshi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan hususan katika siku za hivi karibuni.

Duru za Palestina zimetangaza kuwa, ndege isiyo na rubani ya jeshi la Israel imeshambulia viunga vya kambi ya Tulkarm katika Ukingo wa Magharibi, na kwamba jeshi la Israel limepeleka askari zaidi katika mji wa Jenin.

Vyanzo hivyo vimeripoti kwamba, mashambulizi dhidi ya mji wa Tulkarm na vitongoji vyake yanaendelea kwa siku ya ishirini mfululizo, na kwamba nyumba za karibu na kambi ya wakimbizi ya Tulkarm zinavamiwa na kufanywa vituo na ngome za kijeshi.

Wanajeshi wa Israel wakiwashambulia Wapalestina, Ukingo wa Magharibi

Wavamizi wa Kizayuni wamezidisha mzingiro wa wakazi hao, na wanawazuia kwenda kupata mahitaji yao muhimu. Mashambulizi dhidi ya mji wa Jenin na kambi yake ya wakimbizi pia yanaendelea kwa siku ya ishirini na sita. Hadi sasa mashambulio haya yameua shahidi Wapalestina 25 na kujeruhi makumi ya wengine, mbali na kuharibu miundo mbinu ya maeneo hayo. 

Wakati huo huo, Shirika la Hilali Nyekundu ya Palestina limetangaza kuwa watu kadhaa wamejeruhiwa na kupelekwa hospitalini kutokana na mashambulizi ya walowezi dhidi ya raia wa Wapalestina katika eneo la "Al-Minya" huko Bait Laham (Bethlehem). Kwa upande mwingine, jeshi la Israel limetuma zana zaidi za kijeshi na wanajeshi katika mji wa Jenin ulioko kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi. Vyanzo vya Wapalestina pia vimeripoti shambulio la wanajeshi wa Israel kwenye kambi ya "Al-Dahshiyya" huko Bait Laham.

Vikosi vitatu vya jeshi vya jeshi la Israel vinaendelea na mashambulizi katika maeneo matatu tofauti kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi, ambayo ni Jenin, Tulkarm na Tubas, na Shirika la Usalama wa Ndani la Israel, Shin Bet, pia linashiriki katika operesheni hizo likishirikiana na jeshi.

Jinai za mauaji ya kimbari yaliyoanzishwa utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza baada ya makundi ya muqawama wa Palestina kuanzisha Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa, tarehe 7 Oktoba 2023, zinatekelezwa sasa katika eneo la kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Jeshi la Israel limezidisha mashambulizi dhidi ya kambi za wakimbizi wa Palestina kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, kwa lengo la kukabiliana na makundi ya Kipalestina na kuzuia operesheni zozote dhidi ya walowezi wa Kizayuni.

Lengo jingine ovu la Wazayuni ni kuzidisha na kuendeleza hali mbaya ya wakimbizi wa Kipalestina katika eneo la kaskazini la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Uungaji mkono na mshikamano kamili wa wananchi wa Palestina kwa makundi ya Muqawama, licha ya mashambulizi ya kikatili ya Wazayuni, si tu kwamba haujakoma, bali leo hii umaarufu wa Hamas na makundi ya wapigania ukombozi wa Palestina katika eneo la Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan umeongezeka sana.

Katika mazingira hayo, utawala wa Kizayuni kutokana na kukata tamaa mbele ya muqawama wa Palestina na kushindwa kutimiza njama na malengo yake maovu huko Gaza, umeamua kuzusha mgogoro katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Umoja wa Mataifa umeonya katika ripoti yake kwamba mashambulizi ya jeshi la Israel kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi "yameharibu kambi za wakimbizi wa Kipalestina katika eneo hilo na kuwalazimisha watu kuhama mara kwa mara." Umoja wa Mataifa umeitaja hali ya ukimbizi wa Wapalestina huko kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi, kutokana na mashambulizi ya jeshi la Israel, kuwa ni tukio baya na la kikatili zaidi la Wapalestina kuhama makazi yao katika miongo ya hivi karibuni.

Wapalestina wa Ukingo wa Magharibi wanafukuzwa katika makazi yao

Jaribio la kuwafukuza kwa nguvu Wapalestina katika makazi yao ndilo lengo kuu la mpango wa Wazayuni wa kupanua ujenzi wa vitongoji vya walowezi, ambao bado haujafanikiwa huko Gaza. Katika mazingira haya, Wazayuni wanataka kuzidisha vita katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ili eti kufidia kushindwa kwao huko Gaza.

Hata hivyo, vita vya Gaza vimeonyesha kuwa, utambulisho wa Wapalestina hauwezi kuangamizwa kwa watu kufukuzwa katika makazi yao na kwa mauaji ya kimbari. Kwa sababu hiyo, mipango yote ya kuhamishwa watu kwa mabavu, vita na mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina, ikiwa ni pamoja na vita vya Israel vinavyoendelea sasa katika Ukingo wa Magharibi, imeshindwa hata kabla kuanza kwake.