Kushindwa Trump katika "Kamari ya Jumamosi Adhuhuri"
Jumamosi adhuhuri pia imekuja na kupita na licha ya Hamas kukataa kuwaachilia huru mateka wote wa Kizayuni kama alivyotaka Rais Donald Trump wa Marekani, rais huyo ameshindwa kutekeleza tishio lake la kuanzisha Jahannam huko Gaza.
Huku akitangaza upinzani wake mkali kwa mchakato wa kubadilishana taratibu wafungwa na mateka kati ya Israel na Hamas, Trump alitishia kwamba ikiwa Hamas haingewaachilia mateka wote kufikia saa sita mchana Jumamosi Februari 15, usitishaji mapigano huko Gaza ungefikia kikomo na kwa kauli yake mwenyewe, Jahannam ingeibuka katika eneo hilo.
Hata hivyo, Hamas ilipinga kuachiliwa mara moja mateka wote, na bila kujali vitisho vya rais wa Marekani, ikatangaza kwamba itaheshimu makubaliano yaliyofikiwa ya kuachiliwa idadi ndogo ya mateka wa Israel mkabala wa kuachiliwa huru idadi kubwa ya wafungwa wa Kipalestina. Katika muktadha huo, Hamas iliwaachilia huru mateka watatu wa Israel saa sita mchana siku ya Jumamosi, Februari 15, nayo Israel kwa upande mwingine ikawaachia huru wafungwa 369 wa Kipalestina. Mabadilishano hayo na kuendelea usitishaji mapigano kunathibitisha wazi kushindwa Rais wa Marekani katika mchezo wa kamari ya masuala ya usalama na siasa.
Bila shaka, ili kufunika fedheha ya kushindwa huko, Trump ameurusha mpira katika uwanja wa Wazayuni kwa kusema kuwa utawala wa Israel ndio unapaswa kuamua iwapo utaendelea na usitishaji vita huko Ghaza au la. Wakati huo huo, amedai kuwa uamuzi wowote utakaochukuliwa na utawala huo kuhusu suala hilo utaungwa mkono na serikali ya Marekani. Lakini haionekani kuwa Israel ina nia ya kuanzisha tena vita huko Gaza, kwa uchache sio katika mazingira ya sasa. Mojawapo ya sababu ni kwamba kuanzishwa tena vita kutaipelekea Hamas kusimamisha mchakato wa kuachilia huru mateka, jambo ambalo bila shaka litaongeza mashinikizo ya kisiasa dhidi ya serikali ya Benjamin Netanyahu ndani ya utawala ghasibu wa Israel. Kwa namna ambayo uwezekano wa kuuawa au kujeruhiwa mateka waliosalia mikononi mwa Hamas utaigharimu pakubwa kisiasa serikali ya Israel.
Wakati huo huo, hakuna matarajio yoyote ya kufanikiwa Netanyahu katika medani ya vita huko Gaza, kwa uchache katika muda mfupi ujao. Kwa msaada wa Marekani na Ulaya, Israel ilifanya kila aina ya jinai ilizoweza huko Gaza katika miezi 15 na kuliangamiza kabisa eneo hilo, lakini pamoja na hayo haikuweza kuushinda muqawama wa watu wa Palestina. Kuwepo kwa vikosi vya Hamas katika pembe zote za Gaza katika siku za baada ya kusitishwa mapigano katika ukanda huo kumethibitisha kwamba Hamas bado ina nguvu na ushawishi mkubwa na kwamba mauaji ya umati yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika eneo hilo hayakudhuru muundo wa kijeshi na mapigano wa vikosi vya kundi hilo la muqawama wa Palestina.
Kwa upande mwingine, ingawa Trump alitishia kwamba angeanzisha Jahannam huko Gaza, lakini utekelezaji wake umetiliwa shaka kubwa. Bila shaka, si kwa sababu Wamarekani hawawezi kuanzisha Jahannam huko Gaza, lakini kimsingi, kwa kuanzisha mashambulizi na mauaji ya kutisha ya Israeli huko Gaza mnamo Oktoba 7, 2023, tayari Jahannam ilikuwa imeshaanzishwa kwa msaada wa Wamarekani, lakini pamoja na hayo muqawama wa Palestina haukushindwa bali ndio uliibuka mshindi. Hivyo ni wazi kuwa muqawama wa Wapalestina hautashindwa kwa kukaririwa vitisho vya kuanzishwa tena Jahannam na Israel pamoja na Marekani huko Gaza.
Ni wazi kuwa kushindwa Trump katika bwabwaja zake za "Kamari ya Adhuhuri"; si tu kumemshushia hadhi binafsi shakhsia huyo, bali pia kumedhuru heshima ya ofisi ya rais wa Marekani.