Askofu Mkuu wa Quds: Palestina, kamwe haitomsahau Nasrullah
(last modified Fri, 21 Feb 2025 06:51:45 GMT )
Feb 21, 2025 06:51 UTC
  • Askofu Mkuu wa Quds: Palestina, kamwe haitomsahau Nasrullah

Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiorthodoksi la Ugiriki katika mji mtukufu wa al-Quds unaokaliwa kwa mabavu, Atallah Hanna, amemuenzi na kumsifu aliyekuwa Kiongozi wa Harakati ya Muqawama ya Hizbullah nchini Lebanon, Sayyid Hassan Nasralluh, akisisitiza kuwa watu wa Palestina daima wataendelea kuwa waaminifu kwake kwa namna alivyojitolea muhanga.

Askofu Hanna ametoa ujumbe wa kumuenzi na kumuomboleza Sayyid Nasrullah kabla ya maziko makubwa ya Katibu Mkuu huyo wa zamani wa Hizbullah yanayotazamiwa kufanyika siku ya Jumapili nchini Lebanon; akimtaja kuwa "Kiongozi wa Mashahidi wa Umma wa Kiislamu."

"Baada ya siku chache, Lebanon itashuhudia tukio la aina yake na la kihistoria - maziko ya Sayyid Hassan Nasrullah na mashahidi wenzake," imesema sehemu ya ujumbe wa Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiorthodoksi katika mji wa Quds. 

Hizbullah iliakhirisha maziko ya Sayyid Nasrullah kwa sababu ya hofu ya mashambulizi zaidi kutoka Israel wakati wa marasimu hayo. Sayyid Nasrullah aliuawa shahidi katika shambulizi kubwa la anga la Israel kwenye vitongoji vya kusini mwa Beirut mnamo Septemba 27, 2024, wakati jeshi la Kizayuni liliposhadidisha kampeni yake dhidi ya Hizbullah. 

Askofu Hanna amesema, "Kutoka al-Quds, tunasimama kwa heshima na taadhima kwa ajili ya kujitolea kwake (Nasrullah) muhanga, na vile vile wanamapambano zake, ambao walisimama na Palestina, wakaitetea, na kulipa gharama kubwa kwa ajili yake." 

"Tunasalia watiifu kwa dhabihu hizi, na watu wote wa Palestina wanasalia kuwa waaminifu kwa kujitolea kwingi Mtukufu (huyo) na wafuasi wake," Askofu Hanna amesema, akimzungumzia Shahidi Nasrullah.