Nini kinajiri hivi sasa huko Syria?
Miezi mitatu baada ya kuanguka utawala wa Bashar al-Assad, Syria inashuhudia duru mpya ya vurugu na mivutano kati ya serikali ya mpito inayotawala nchi hiyo na makundi upinzani katika maeneo mbalimbali nchini humo.
Miji ya Latakia na Tartus katika mikoa ya pwani ya Syria tangu Alhamisi iliyopita imekumbwa na mapigano makali kuwahi kutokea katika miongo ya karibuni. Mikoa hiyo miwili, yenye wakazi zaidi ya milioni mbili na akthari yao wakiwa ni jami ya wachache ya Maalawi, haikushiriki katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria.
Yaliyojiri siku kadhaa zilizopita katika mikoa hiyo ya pwani yanaweza kutajwa kuwa ni mwendelezo wa hali ya mvutano katika mikoa ya kusini na mashariki mwa Syria. Katika jimbo la Al Suwayda linalokaliwa na jamii ya Wadruzi, mvutano umekuwa ukiongezeka kwa wiki kadhaa sasa kati ya jamii hiyo na serikali inayotawala huko Damascus.
Mapigano mapya yalianza baada ya shambulio la Machi 6 mwaka huu wakati watu wenye silaha waliposhambulia kambi kadhaa za vikosi vya usalama wa umma karibu na mji wa Bait Anna huko Latakia, ambapo wapiganaji 16 wa kundi la Tahrir al-Sham waliuawa katika shambulio hilo. Kufuatia shambulio hilo, vikosi vyenye mfungamano na Jolani vilitumwa katika eneo la tukio ili kupambana na watu wenye silaha.
Eneo jingine lililoshuhudia mapigano makali ni Jabla karibu na Tartus ambalo limekuwa kituo cha kamandi cha vikosi vya upinzani. Baadhi wanamgambo wa Kanali Sohail Hassan pia walionekana katika mapigano hayo, jambo linaonyesha kuongezeka mchakato wa kuwapa silaha wanamgambo wenye mfungamano na jeshi la zamani la Syria, ambao aghalabu yao wanatoka katika kikosi maalumu na askari jeshi wasomi na wa usalama; na inaonekana kuwa Maher Assad amekusudia kuifanya mikoa hiyo miwili kuwa kitovu cha machafuko.
Kwa msingi huo, jiografia ya mapigano yanayoendelea huko Syria inaonyesha kuwa yanajiri katika maeneo ya jamii ya Maalawi, wafuasi wa utawala wa zamani, na katika baadhi ya maeneo ya Wakurdi. Aghalabu ya makamanda wa jeshi na vikosi vya usalama wa serikali ya Bashar al Assad wamerejea katika mikoa hiyo miwili na kuanzisha kambi ya upinzani kupitia maandamano ya mitaani, harakati za kijeshi na kiusalama dhidi ya utawala wa Ahmad al Jolani. Inaonekana kuwa ikiwa imepita miezi 3 tangu kuangushwa utawala wa Bashar al Assad, kunashuhudiwa ukandamizaji mkubwa unaofanywa na serikali ya muda hususan dhidi ya Maalawi, na kwa upande wa pili, kupatiwa silaha na kujiratibu upya maafisa wa jeshi wa utawala uliopita ni sababu ya kushuhudiwa duru mpya ya mapigano katika maeneo mbalimbali ya Syria.
Ahmed al Sharaa (Jolani) kiongozi wa serikali ya muda ya Syria ametishia kuwakandamiza na kuwaadhibu wapinzani wake katika hotuba aliyoitoa kwa njia ya video. Amesema, Syria ni moja tu, na kwamba shambulio lolote katika ardhi ya nchi hiyo ni shambulio dhidi ya nchi nzima na kudai kuwa: "Hatutamvumilia yeyote anayeshambulia raia au taasisi za serikali." Jolani amewataka wapinzani kuweka chini silaha zao.
Nukta muhimu ni kuwa, katika hali ambayo wapiganaji wa Jolani wamezidisha hujuma na vitendo vya mabavu na kuuwa mamia ya watu, sambamba na kuwanyonga watu wengi, lakini nchi ajinabi ambazo huko nyuma zilijinadi kuwa watetezi wa haki za binadamu huko Syria hadi sasa zimenyamaza kimya na hazijatoa radiamali yoyote mkabala wa vitendo hivyo viovu na ukandamizaji mkubwa unaoshuhudiwa huko Syria.