UN: Mashambulizi ya Israel yamepelekea Wapalestina 40,000 kupoteza makazi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i123752-un_mashambulizi_ya_israel_yamepelekea_wapalestina_40_000_kupoteza_makazi
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) limesema kuwa uvamizi wa Israel katika Ukingo wa Magharibi umesababisha "uhamishaji mkubwa wa watu" ambao haujawahi kushuhudiwa tangu vita vya mwaka 1967, vilivyosababisha kukaliwa kwa mabavu ardhi ya Palestina.
(last modified 2025-03-11T01:02:37+00:00 )
Mar 11, 2025 01:02 UTC
  • UN: Mashambulizi ya Israel yamepelekea Wapalestina 40,000 kupoteza makazi

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) limesema kuwa uvamizi wa Israel katika Ukingo wa Magharibi umesababisha "uhamishaji mkubwa wa watu" ambao haujawahi kushuhudiwa tangu vita vya mwaka 1967, vilivyosababisha kukaliwa kwa mabavu ardhi ya Palestina.

Katika ripoti yake mpya, UNRWA imekadiria kuwa mashambulizi ya Israel katika wiki chache zilizopita yamesababisha angalau Wapalestina 40,000 kupoteza makazi yao, wengi wao wakiwa ni wakazi wa kambi za wakimbizi katika maeneo yanayokaliwa kimabavu katika Ukingo wa Magharibi.

Mashambulizi hayo makubwa ni ya muda mrefu zaidi kuwahi kufanywa na Israel katika Ukingo wa Magharibi tangu Intifada ya pili ya Wapalestina mwanzoni mwa miaka ya 2000, huku ripoti ikieleza kuwa “yamesababisha uhamishaji mkubwa zaidi wa watu tangu vita vya 1967.”

UNRWA pia imeonya kuwa matamshi ya viongozi wa Israel yanaashiria kuwa operesheni za kijeshi za utawala huo zinaweza kuendelea kwa muda usiojulikana, huku Wapalestina wakizuiwa kurejea kwenye kambi zao za wakimbizi katika Ukingo wa Magharibi.

Jeshi katili la utawala dhalimu wa Israel lilianzisha mashambulizi yake dhidi ya Ukingo wa Magharibi mnamo Januari 21, likidai kuwa linawalenga wapiganaji wa Battalioni ya Jenin.

Tangu Oktoba 7, 2023,  utawala dhalimu wa Israel umeshadidisha mashambulizi yake katika Ukingo wa Magharibi sambamba na vita vyake vya mauaji ya halaiki dhidi ya Ukanda wa Gaza. Tangu wakati huo, vikosi vya Israel vimewaua Wapalestina wasiopungua 930 na kuwajeruhi wengine karibu 7,000 katika maeneo yanayokaliwa kimabavu katika Ukingo wa Magharibi.