Israel inashinikiza nchi za Afrika kuchukua Wapalestina wa Gaza
Utawala ghasibu wa Isarel umeelekeza shirika lake la ujasusi la Mossad kutafuta nchi ambazo zitaafiki mpango wa kupokea idadi kubwa ya Wapalestina watakaohamishwa kwa nguvu kutoka Ukanda wa Gaza.
Maafisa wawili wa Israel wameufahamisha mtandao wa Axios kwamba waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, pia anatafuta njia za kuhamasisha idadi kubwa ya Wapalestina, katika nchi zilizo umbali wa maelfu ya kilimoita.
Maafisa hao na afisa mmoja wa zamani wa Marekani wamedai kwamba mazungumzo tayari yamefanyika na nchi mbili masikini zenye mizozo mashariki mwa Afrika, ambazo ni Somalia na Sudan Kusini, pamoja na nchi nyingine ikiwemo Indonesia.
Maafisa hao wamebaini kwamba Netanyahu alitoa agizo hilo la siri kwa Mossad wiki kadhaa zilizopita.
Ripoti hiyo inadokeza kwamba Israeli inafuatilia njama hiyo ya kuwafukuza Wapalestina kutoka Gaza na wakati huo huo inaendeleza vita huku ikitoa amri kwa Wapalestina kuondoka katika baadhi ya maeneo ya Gaza.
Netanyahu na wanasiasa wengine wa Israeli wameapa kukalia kwa mabavu maeneo zaidi ya Gaza.
Takriban asilimia 90 ya wakazi wa Gaza tayari wamehamishwa kutoka makazi yao kutokana na vita, na zaidi ya watu 50,000 wameuawa, wengi wakiwa ni wanawake na watoto.
Wapalestina wanapinga kwa nguvu juhudi zozote za kuwaondoa kutoka ardhi yao ya jadi licha ya masaibu waliyoyapitia.
Rais wa Marekani Donald Trump alifichua kwa mara ya kwanza mpango wake wa maangamizi ya kikabila Gaza mnamo Februari.
Kulingana na mpango huo, Wapalestina amba ni wenyeji asili wa Gaza watahamishwa kwa nguvu kwenda Jordan na Misri, bila kujali ridhaa yao au serikali za Jordan na Misri.
Tangu kuanza kwa mauaji ya kimbari ya Israeli huko Gaza, makamanda wengi wa Israeli pia wamekuwa wakitoa wito wa kusafisha kikabila Gaza, ikiwa ni pamoja na mawaziri wa utawala wa sasa wa Israel.
Mpango wa kusafisha kikabila Gaza umepingwa vikali na mashirika ya kutetea haki za binadamu na serikali duniani kote, ikiwa ni pamoja na hata baadhi ya washirika wa Israel, kama Ujerumani.