Jeshi la Yemen laangusha ndege ya kivita ya Marekani aina ya MQ-9
(last modified Tue, 01 Apr 2025 03:07:08 GMT )
Apr 01, 2025 03:07 UTC
  • Jeshi la Yemen laangusha ndege ya kivita ya Marekani aina ya MQ-9

Jeshi la Yemen limetangaza kuangusha  ndege ya kivita ya isiyo na rubani au droni ya Marekani aina ya MQ-9 katika Mkoa wa Ma’rib, ikiwa ni droni ya 16 kuangushwa na nchi hiyo tangu Oktoba 7, 2023.

Taarifa ya Jeshi la Yemen iliyotolewa Jumatatu usiku imesema: "Katika kulipiza kisasi uvamizi wa Marekani dhidi ya nchi yetu, kikosi cha ulinzi wa anga kimefanikiwa kuangusha droni ya Marekani aina ya MQ-9 Reaper wakati ilipokuwa ikitekeleza operesheni za uhasama katika anga ya Mkoa wa Ma’rib, kwa kutumia kombora ambalo limeundwa hapa nchini."

Taarifa hiyo imesema: "Hii ni droni ya kumi na sita ambayo kikosi chetu cha ulinzi wa anga kimefanikiwa kuangusha wakati wa Vita vya Ushindi Ulioahidiwa na Jihadi Tukufu kwa ajili ya kuunga mkono Gaza."

Droni moja ya MQ-9 Reaper inagharimu takribani dola milioni 33.

Jeshi la Yemen limethibitisha kuwa "litaendelea kuzuia meli za Israel kupita katika Bahari Nyekundu na Bahari ya Kiarabu na litaendelea kuunga mkono watu wa Palestina hadi uvamizi dhidi ya Gaza utakapoisha na mzingiro kuondolewa."

Taarifa hiyo imebainisha kuwa, "Vikosi vya Jeshi la Yemen havitasita, kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, kutekeleza operesheni zaidi za kujihami dhidi ya meli zote za kivita za adui katika siku zijazo."

Ndege ya kivita ya Markani isiyo na rubani aina ya MQ-9 Reaper

Jumapili usiku, Marekani ilitekeleza mashambulizi mengine ya uhasama dhidi ya Yemen kwa lengo la kulazimisha nchi hiyo ya Kiarabu kusitisha msaada wake kwa Wapalestina wa Gaza.

Ndege za kivita za Marekani zilifanya mashambulizi makali 13 ya anga katika mji mkuu wa Yemen, Sana’a.

Wayemen wamekuwa wakilenga ngome za utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani kwa ajili ya kuwaunga mkono Wapalestina wa Gaza tangu utawala wa Kizayuni ulipoanzisha vita vyake vya kuangamiza dhidi ya Gaza mnamo Oktoba 7, 2023, na kwa kujibu uvamizi wa Marekani na Uingereza dhidi ya nchi yao.

Operesheni hizo zimefanikiwa kufunga bandari ya Eilat kusini mwa ardhi zilizokaliwa kwa mabavu, na kusababisha hasara kubwa za kiuchumi kwa Wazayuni.

Jeshi la Yemen limesema halitasitisha mashambulizi yake hadi mashambulizi ya ardhini na ya anga ya Israel dhidi ya Gaza yatakapokoma.