Wakati anatumikia kifungo jela, Imran Khan ateuliwa kuwania Tuzo ya Amani ya Nobel
Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistani Imran Khan aliyefungwa jela, ameteuliwa kuwania Tuzo ya Amani ya Nobel kwa "kazi aliyofanya kuhusiana na haki za binadamu na demokrasia nchini Pakistan". Hayo yameelezwa katika tamko lililotolewa na chama cha siasa cha Norway Partiet Sentrum.
Khan, ambaye ni mwanzilishi wa chama cha upinzani cha Pakistan Tehreek-e-Insaf (PTI), amefungwa jela tangu Agosti 2023. Mnamo mwezi Januari, alihukumiwa kifungo cha miaka 14 katika kesi ya 'ufisadi' kwa kinachodaiwa kuwa ni matumizi mabaya ya mamlaka, ikiwa ni hukumu ya nne dhidi yake.
Kesi alizohukumiwa kabla, ya zawadi za serikali, uvujishaji wa taarifa za siri, na ndoa isiyo halali zilikuja kubatilishwa au kusimamishwa baadaye.
Nyota huyo wa zamani wa kriketi aliyegeuka kuwa mwanasiasa aliondolewa madarakani Aprili 2022 baada ya kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye na Bunge. Hata hivyo Khan amekana mashtaka yote dhidi yake akisisitiza kuwa yamechochewa na sababu za kisiasa.../