Vikosi vya Yemen vyashambulia Israel na meli za kivita za Marekani
Vikosi vya Jeshi la Yemen vimeendesha msururu wa operesheni kulipiza kisasi kutokana na mashambulizi yanayoendelea ya Marekani katika nchi hiyo ya Kiarabu, vikishambulia ngome muhimu za Isarel katika ardhi zinazikaliwa kwa mabavu pamoja na meli za kivita za Marekani katika Bahari Nyekundu ya Kaskazini na Bahari ya Arabia.
Brigedia Jenerali Yahya Saree, msemaji wa jeshi la Yemen, amesema Jumapili asubuhi kuwa vikosi vya Yemen vilitekeleza shambulizi la kulipiza kisasi dhidi ya eneo la kimkakati katika mji wa Ashkelon ulioko kusini mwa maeneo yanayokaliwa kwa mabavu, kwa kutumia droni ya kivita ya kizalendo aina ya Yaffa.
Vilevile, Jeshi la Yemen limeshambulia ngome ya kijeshi ya Israel katika mji wa bandari wa Eilat kwa kutumia ndege isiyo na rubani iliyotengenezwa ndani ya nchi aina ya Sammad-1.
Jenerali Saree amebainisha kuwa operesheni hizo za kulipiza kisasi pia ni ishara ya mshikamano na Wapalestina walioko katika Ukanda wa Gaza ulioko kwenye mzingiro, huku vita vya kikatili vya mauaji ya halaiki vikielekezwa dhidi ya eneo hilo na Israel vikiendelea.
Zaidi ya hayo, vitengo vya majini na droni vya Jeshi la Yemen vimetekeleza mashambulizi dhidi ya meli ya kubeba ndege za kivita ya Marekani, USS Harry S. Truman, na meli zinazoiandamana nayo katika Bahari Nyekundu, kulipiza kisasi dhidi ya uchokozi unaoendelea wa Marekani dhidi ya Yemen, ambao umesababisha vifo na majeraha kwa raia wengi pamoja na uharibifu wa miundombinu muhimu.
Msemaji wa jeshi la Yemen amesema kuwa vikosi vyao vilishambulia meli za kivita za Marekani kwa kutumia makombora mawili ya kuvamia meli yaliyotengenezwa nchini na droni mbili za kushambulia.
Vikosi vya majini, droni, na makombora vya Yemen pia vililenga meli ya kubeba ndege ya kivita ya Marekani, USS Carl Vinson, pamoja na meli zinazoiandamana katika Bahari ya Arabia kwa kutumia makombora matatu ya masafa ya kati na droni nne.
Jenerali Saree amesisitiza: “Vikosi vya Jeshi la Yemen vitaendelea na operesheni za kulipiza kisasi dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kasi inayoongezeka wiki na miezi ijayo.
Halikadhalika amesema: "Vikosi vya Yemen vitaendeleza mashambulizi yao katika Bahari Nyekundu na Bahari ya Arabia, vikilenga majeshi vamizi. Mashambulizi ya anga ya Marekani, hata kama yatakuwa mengi kiasi gani, hayatavifanya vikosi vya Yemen kuacha kuunga mkono Wapalestina waliodhulumiwa huko Gaza hadi uchokozi huo utakapositishwa na mzingiro mkali kuondolewa kabisa."