Kubadilika mtazamo wananchi wa Marekani kuhusu Israel, Palestina na Hamas
(last modified Thu, 24 Apr 2025 03:31:34 GMT )
Apr 24, 2025 03:31 UTC
  • Kubadilika mtazamo wananchi wa Marekani kuhusu Israel, Palestina na Hamas

Wakati vita vya Ghaza vinaendelea na utawala wa Kizayuni umeshadidisha mauaji ya wanawake na watoto wa Palestina, mtazamo na mwelekeo wa wananchi wa Marekani kuhusuu Israel, Palestina na Hamas nao unaendelea kubadilika. Haya yamebainika katika chunguzi mpya za maoni zilizofanywa nchini Marekani.

Chunguzi hizo za maoni zilizofanywa hivi karibuni kabisa na shirika la Gallup zinaonesha kuwa, uungaji mkono wa wananchi wa Marekani kwa Israel umefikia kiwango cha chini kabisa. Kwa mujibu wa takwimu za taasisi hiyo, ni asilimia 46 tu ya watu wazima wa Marekani waliounga mkono Israel wakati walipoulizwa: "Je, unamuonea huruma nani zaidi, Waisraeli au Wapalestina?" huku asilimia 33 wakijibu kwamba wanawaunga mkono zaidi Wapalestina. Hiki ndicho kiwango cha chini zaidi cha uungaji mkono wa Israel kwenye safu za wananchi wa Marekani katika kipindi cha miaka 25. Aidha huu ni mwaka wa pili mfululizo ambapo uungaji mkono huo unaporomoka. Mwaka jana 2024, takwimu hizo zilikuwa ni asilimia 51 na ilirekodi kiwango cha chini kabisa cha uungaji mkono kwa Israel tangu mwaka 2001. Hivi sasa pia na tangu mwanzoni mwa mwaka 2025, idadi ya wananchi wa Marekani wanaoiunga mkono Israel imezidi kuporomoka. Inafaa kuashiria hapa kwamba, asilimia 75 ya wanachama wa chama cha Trump cha Republican ni waungaji mkono sugu wa jinai za Israel huku asilimia 21 ya wanachama wa chama cha Democratic wakiwa ndio waungaji mkono wa Israel. 

Jambo lingine ni kwamba asilimia 32 ya Wamarekani wana mitazamo chanya kuhusu Palestina, ni hiyo ni idadi kubwa sana ikilinganishwa na mwaka jana. Huu ni uungaji mkono wa hali ya juu kabisa ambao Wapalestina wamewahi kuupata kutoka kwa wananchi wa Marekani.

Wimbi kubwa la wananchi wa Marekani wanailaani Israel na kuiunga mkono Palestina

 

Mbali na kupanda sana kiwango cha uungaji mkono wa Marekani kwa Wapalestina, mtazamo jumla wa wananchi wa Marekani kuhusu Hamas pia ni kinyume na matarajio ya wanasiasa wa nchi hiyo ambao wanafanya njama kubwa sana za kueneza chuki dhidi ya harakati hiyo ya Muqawama ya Palestina. Kwa mujibu wa uchunguzi mpya wa maoni uliofanywa na Taasisi ya Harvard-Harris mwezi Machi 2025, asilimia 48 ya vijana wa Marekani wenye umri wa miaka 18 hadi 24 wanaiunga mkono Hamas. Hili ndilo kundi la jamii ya Marekani linaloiunga mkono sana Hamas. Lakini kati ya wale wenye umri wa miaka 25 hadi 64, uungaji mkono kwa Israel ni mkubwa kuliko Hamas kwa asilimia 60, ingawa ndani ya kundi hilo pia, asilimia 24 wanaamini kuwa Hamas inapaswa kuendelea kutawala Ghaza. Hata hivyo, kiwango cha juu zaidi cha uungaji mkono kwa Israel bado kinatoka kwa Wamarekani wenye umri wa kuanzia miaka 65 na kuendelea. Asilimia 93 ya vizee hivyo vya Marekani bado vina kasumba ya kuiunga mkono Israel.

Mashambulio ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ghaza, mauaji ya halaiki ya Wapalestina na kuendelea jinai kubwa mno za utawala ghasibu wa Israel wakati wa vita vya Ghaza ni mambo ambayo yamezusha wimbi kubwa mno la maandamano ya wananchi na harakati ya wanafunzi huko Marekani kwa namna ambayo haijawahi kutokea katika historia ya nchi hiyo. Bila ya shaka yoyote misimamo ya wananchi wa Marekani ni tofauti na misimamo ya watawala wanaoongoza kiimla nchini humo. Hisia zozote za kibinadamu haziwezi kuvumilia na kunyamazia kimya jinai za kutisha zinazofanywa na Wazayuni huko Palestina na hasa Ghaza. Mbali na wanafunzi, kwa mara ya kwanza, idadi kubwa ya maprofesa, wahadhiri na wasimamizi wa vyuo vikuu vya Marekani nao walijiunga na waandamanaji kulaani jinai za Israel na kuwaunga mkono Wapalestina. 

Wimbi hili kubwa la uungaji mkono wa Palestina halijawahi kushuhudiwa kwenye historia ya Marekani

 

Suala muhimu katika kadhia hii nzima, ni huko kuongezeka uungaji mkono wa wananchi wa Marekani kwa Wapalestina na hata kwa Hamas suala ambalo kabla ya Operesheni ya Kimbunga cha Al Aqsa na jinai za Israel zilizoanzia tarehe 7 Oktoba 2023 lilikuwa ni dogo sana katika jamii ya Marekani. Kinachotia moyo zaidi ni kwamba kizazi cha vijana wa Marekani kimeamka hivi sasa na asilimia kubwa ya vijana wa nchi hiyo wanaiunga mkono Palestina na HAMAS na wanalaani jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel. Ukitoa kasumba ya vizee walioshibishwa na propaganda chapwa za huko nyuma, sehemu kubwa ya wananchi wa Marekani wanazidi kuamka na kuwa na msimamo tofauti hivi sasa kuhusu Israel, Palestina na HAMAS, na hayo ni katika mafanikio makubwa ya operesheni ya Kimbunga cha al Aqsa iliyoongozwa na HAMAS mwezi Oktoba 2023.