Serikali ya Jordan yaipiga marufuku harakati kongwe ya Kiislamu ya Ikhwanul-Muslimin
(last modified Thu, 24 Apr 2025 04:14:08 GMT )
Apr 24, 2025 04:14 UTC
  • Serikali ya Jordan yaipiga marufuku harakati kongwe ya Kiislamu ya Ikhwanul-Muslimin

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jordan ametangaza kuwa utawala huo wa kifalme umeipiga marufuku harakati ya Kiislamu ya Ikhwanul-Muslimin na kuielezea "itikadi" yake inayohubiri kuwa sasa ni 'haramu' kisheria nchini humo.

Mazin Abdellah Hilal al-Farrayeh alitangaza marufuku hiyo jana Jumatano katika mkutano na waandishi wa habari, akisema "shughuli yoyote ya kundi hili, bila kujali ni ya aina gani, inachukuliwa kuwa ni ya uvunjaji sheria".
 
Al-Farrayeh ameongeza kuwa, ofisi na majengo ya harakati ya Ikhwanul-Muslimin sasa yatafungwa, na mali zake zitazuiliwa.
 
Waziri wa mambo ya ndani wa Jordan amebainisha kuwa uhusiano na maingiliana ya aina yoyote na kundi hilo sasa yamepigwa marufuku na kwamba uenezaji wa "itikadi" yake utapelekea mtu kufunguliwa mashtaka ya kosa la jinai.
 
Harakati ya Ikhwanul-Muslimin ilianzishwa mjini Cairo, Misri mwaka 1928 na ni moja ya makundi makubwa zaidi na mashuhuri zaidi yanayohubiri Uislamu wa kisiasa duniani.

Harakati hiyo kongwe ya Kiislamu imekuwa kwa muda mrefu ikiendesha harakati zake kwa njia za amani zinazoshajiisha kushiriki katika siasa za kidemokrasia, lakini inachukiza mbele ya tawala nyingi za kiimla katika Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini.

Katika miaka ya karibuni, tawi la Ikhwanul-Muslimin nchini Jordan limekuwa halisikiki sana, ingawa wanachama wake na watu wenye mfungamano nalo wamekuwa wakilaani vikali vita vya kinyama na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ghaza na kuwatolea wito Waarabu wawaunge mkono na kuwasaidia wananchi hao wanaodhulumiwa.

Utawala wa kifalme wa Jordan ni miongoni mwa nchi chache za Kiarabu zenye uhusiano rasmi wa kidiplomasia na utawala haramu wa Israel.../