Hizbullah ya Lebanon yaeleza kwa msisitizo: Hatutasalimu amri mbele ya njama za Israel na Marekani
(last modified Tue, 29 Apr 2025 07:13:26 GMT )
Apr 29, 2025 07:13 UTC
  • Hizbullah ya Lebanon yaeleza kwa msisitizo: Hatutasalimu amri mbele ya njama za Israel na Marekani

Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon Sheikh Naim Qassem amezungumzia shambulio la hivi karibuni la utawala wa Kizayuni kwenye viunga vya kusini mwa mji mkuu wa Lebanon, Beirut, na akasema: "shambulio hili limefanywa kwa idhini na uungaji mkono wa Marekani."

Katika hotuba aliyotoa usiku wa kuamkia leo Sheikh Naim Qassem, ameashiria vipaumbele vitatu vikuu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Lebanon na akasema: "kipaumbele cha kwanza ni kusimamisha uvamizi na uchokozi wa utawala wa Kizayuni katika ardhi ya Lebanon, kisha kuondolewa majeshi ya utawala huo na kuachiwa huru mateka".

Ikinukuu televisheni ya Al-Alam, Pars Today, imeripoti kuwa, Katibu Mkuu wa Hizbullah amesisitizia msimamo wa harakati hiyo ya Muqawama wa kuendelea kuheshimu makubaliano ya usitishaji vita na akaongezea kwa kusema: "Muqawama umetekeleza makubaliano hayo kikamilifu na haujawahi kuyakiuka katu, hali ya kuwa utawala wa Kizayuni hadi sasa umeshayakiuka makubaliano hayo zaidi ya mara elfu tatu, huku Marekani ikiwa kitu kimoja na Israel na kwa hiyo inabeba dhima ya hatua hizo".

Sheikh Naim Qassem amekumbusha kwa kusema: lengo kuu la utawala wa Kizayuni ndani ya Lebanon ni kuidhibiti nchi hiyo na kuidhoofisha; na akaendelea kubainisha kuwa waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni Benjamin Netanyahu anakabiliwa na hali ngumu na changamoto kubwa. 

Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema: "katika kilele cha vita hatukumruhusu Netanyahu afanye atakavyo na sisi hatutarudi nyuma kwenye hata moja katika matakwa yetu.

Aidha, Sheikh Naim Qassem ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Kiongozi Muadhamu na wananchi wa Iran kwa kuisaidia Lebanon.../