Zaidi ya wahudumu 1400 wa sekta ya tiba Gaza wameuawa na Israel
(last modified Thu, 01 May 2025 03:45:46 GMT )
May 01, 2025 03:45 UTC
  • Zaidi ya wahudumu 1400 wa sekta ya tiba Gaza wameuawa na Israel

Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Gaza imetangaza kuwa mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Israel yameua mamia ya madaktari na wahudumu wa afya katika eneo hilo linalozingirwa.

Mkurugenzi wa hospitali moja huko Gaza alitangaza kuporomoka kwa mfumo wa huduma za afya huko Gaza, na kuongeza: "Hadi sasa, zaidi ya wafanyakazi wa matibabu 1,400 wameuawa shahidi katika ukanda huo."

Marwan al-Hams amesema, mfumo wa afya wa Gaza umekaribia kuporomoka kabisa na unakabiliwa na upungufu mkubwa wa vifaa vya msingi vya matibabu, na madaktari wanalazimika kutekeleza mfumo wa "kipaumbele cha matibabu" kwa wagonjwa, na idadi kubwa ya watu waliojeruhiwa wanaachwa bila matibabu kutokana na ukosefu wa vifaa vya matibabu.

Wizara ya Afya ya Palestina huko Gaza imetoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua zinazohitajika "kuwalinda wafanyakazi wa matibabu na taasisi za afya katika Ukanda wa Gaza."

Katika muda wote wa vita vya mauaji ya halaiki, wanajeshi wa Israel wamekuwa wakizilenga hospitali za Gaza mara kwa mara na kuua sio tu wafanyikazi wa matibabu, lakini pia wagonjwa na Wapalestina na waliokimbilia katika vituo hivyo kwa ajili ya kupata matibabu.

Wakati huo huuo, ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa amenukuliwa akisema tena kuwa, hali ya kibinadamu huko Ghaza ni mbaya sana.

Nalo Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limetangaza kuwa, hali ya watoto huko Ghaza ni mbaya sana na kwamba eneo hilo liko ukingoni mwa kuporomoka.