Mbunge: Israel kamwe haitopata ushindi; Ghaza itakuwa huru
Mbunge mmoja wa zamani wa Bunge la Ulaya, Bi Clare Daly ametoa ujumbe mzito wa kushikamana na Palestina wakati aliposhiriki kwenye Tamasha la Sobh la Kimataifa la Vyombo vya Habari hapa Tehran jana Jumatatu.
Bi Clare Daly ambaye aliwahi kuwa mjumbe wa Bunge la Ulaya kutoka Ireland kuanzia Julai 2019 hadi Julai 2024, ametunukiwa Tuzo Maalumu la Shahidi Ismail Haniyeh ili kuenzi uungaji mkono wake kwa kadhia ya Palestina, haswa wakati wa mauaji ya umati yanayoendelezwa na Israel huko Ghaza.
Mbunge Daly amekuwa mtetezi mkubwa wa mapambano ya ukombozi wa Palestina dhidi ya uvamizi wa Israel na ubaguzi wa rangi na amekuwa akizungumza mengi kuhusu mapambano hayo katika majukwaa ya kimataifa.
Amesema wanafanya juhudi za kupaza sauti ya Muqawama katika kila bara na katika kila nchi wakati ambapo viongozi wa ulimwengu wetu unaodaiwa ni wa kidemokrasia; wao wanasaidia na kuwezesha kufanyika mauaji hayo ya kimbari. Lakini amesema ana matumani kwamba Ghaza itakombolewa, Wapalestina watashinda, na kamwe Israel haitopata ushindi Ghaza.
Tamasha la Kimataifa la Sobh la Vyombo vya Habari, lililoandaliwa na Kitengo cha Matangazo ya Ng'ambo cha IRIB liliendelea jana Jumatatu kwa kuhudhuriwa na makumi ya wageni kutoka nchi za kigeni.
Hilo ni tukio la kila mwaka la vyombo vya habari linalolenga kupaza sauti na simulizi ambazo mara nyingi zinapuuzwa katika vyombo vya habari vya Magharibi, hasa yale yanayohusu harakati za Muqawama za kupambana na majeshi ya madola ya kibeberu. Tamasha la vyombo vya habari la Sobh la mwaka huu limefanyika katika hali ambayo mauaji ya umati yanayofanywa na Israel huko Ghaza yamekaribia kutimiza miezi 20.