Ndege za kivita za Israel zashambulia ghala la chakula la UNRWA huko Jabalia + Video
(last modified Sat, 10 May 2025 06:57:20 GMT )
May 10, 2025 06:57 UTC
  • Ndege za kivita za Israel zashambulia ghala la chakula la UNRWA huko Jabalia + Video

Shirika la Habari la Palestina limetangaza kuwa, ndege za kivita za Israel zimeshambulia ghala la chakula la UNRWA katika kambi ya Jabalia ya kaskazini mwa Ghaza.

Kwa mujibu wa shirika hilo, ndege za kivita za utawala wa Kizayuni wa Israel zimeshambulia ghala la chakula la Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Palestina (UNRWA) katika kambi ya Jabalia ya kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza. Moshi mkubwa umetanda angani juu ya eneo hilo baada ya shambulio hilo la kijinai la Israel.

Katika shambulio hilo, raia 4 wa Palestina wameuawa shahidi na makumi ya wengine wamejeruhiwa, baadhi yao wakiwa ni wanawake na watoto wadogo.

Kabla ya hapo taarifa nyingine zilikukwa zimesema kuwa, watu wanne, mmoja wao akiwa mtoto mdogo, wameauwa shahidi na wengine kadhaa kujeruhiwa kutokana na shambulio la kijinai lililofanywa na adui Mzayuni katika eneo la Hay al-Rimal la magharibi mwa mji wa Ghaza.

Katika kipindi cha saa 24 zilizopita, Wapalestina 27 wameuawa shahidi na 85 kujeruhiwa katika mashambulizi ya kikatili ya Israel huko Ghaza.

Kwa takwimu hizo, idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi katika vita vya Israel dhidi ya Ghaza tangu Oktoba 7, 2023, hadi hivi sasa imeongezeka na kufikia watu 52,787 na idadi ya waliojeruhiwa imefikia Wapalestina 119,349. Idadi hiyo haijumuishi Wapalestina walioko chini ya vifusi na wengine ambao hatima yao haijajulikana.