India na Pakistan zaonyesha nia ya kupunguza mzozo kwa masharti
(last modified Sat, 10 May 2025 12:21:49 GMT )
May 10, 2025 12:21 UTC
  • India na Pakistan zaonyesha nia ya kupunguza mzozo kwa masharti

India na Pakistan leo Jumamosi zimeonyesha nia yao ya kumaliza mzozo wao wa kijeshi iwapo pande zote mbili zitaheshimu uamuzi huo. Hata hivyo, majeshi ya pande hizo mbilii yameendelea kushambuliana kwa silaha za aina mbaliimbali.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistani, Ishaq Dar amesema leo kwamba "Iwapo India itasitisha mzozo, Islamabad itafanya vivyo hivyo."

Akizungumza na kituo cha runinga cha Geo News cha Pakistan, Ishaq Dar amesema: "Kama kutatumiwa akili kiduchu, India itakomesha mashambulizi, na wakikoma, sisi pia tutaacha mashambulizi. Tunataka kwa dhati amani isiyo na ubabe wa nchi yoyote." 

Wakati huo huo, Islamabad imepuuzilia mbali "chaguo la kutumia silaha za nyuklia katika hatua hii" baada ya kutolewa ripoti zinazokinzana kuhusu wito wa mkutano wa chombo cha juu zaidi cha nyuklia nchini humo kujibu mashambulizi ya India.

Waziri wa Ulinzi wa Pakistan, Khawaja Muhammad Asif amesema kuwa chaguo la nyuklia "haliko mezani kwa sasa, lakini ikiwa kutatokea mabadiliko waangalizi pia wataathirika."

Akiongea na Geo News, Asif amesema, "Ninauambia ulimwengu kwamba hili halitaishia kwenye mipaka ya eneo hili, lakini linaweza kuwa na uharibifu mkubwa zaidi. Machaguo yetu yanapungua kutokana na hali ambayo India imeunda."

Awali, televisheni ya CNN iliripoti kwamba mawasiliano ya kwanza ya simu yamefanyika kati ya India na Pakistan na kudai kuwa Islamabad inataka kufanya mkutano na New Delhi.

Mvutano kati ya wapinzani hao wawili wenye silaha za nyuklia ulipamba moto baada ya shambulio la Aprili 22 kwenye kituo maarufu ch watalii huko Kashmir inayodhibitiwa na India ambalo liliua watu 26, wengi wao wakiwa watalii wa Kihindu wa India. New Delhi iliilaumu Pakistan kuwa imeunga mkono shambulio hilo, tuhuma ambayo Islamabad inazikanusha.