Iran: Ni kwa manufaa ya US kulichukulia kwa uzito pendekezo letu
(last modified Mon, 09 Jun 2025 11:29:05 GMT )
Jun 09, 2025 11:29 UTC
  • Iran: Ni kwa manufaa ya US kulichukulia kwa uzito pendekezo letu

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei amesema Tehran hivi karibuni itawasilisha pendekezo lake kuhusu makubaliano ya nyuklia kupitia Oman, akitoa wito kwa Washington kutopoteza fursa hii, na kulichukulia kwa uzito pendekezo la Jamhuri ya Kiislamu.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo Jumatatu, Baghaei amegusia maendeleo ya hivi punde kuhusu mazungumzo ya nyuklia yasiyo ya moja kwa moja kati ya Tehran na Washington na kueleza kuwa: Pendekezo lolote lisilozingatia maslahi ya taifa la Iran halikubaliki.

Marekani na Iran zimefanya duru tano za mazungumzo ya nyuklia tangu Aprili 12 na zinatarajiwa kukutana tena kwa mazungumzo yenye lengo la kufikia makubaliano mapya. Nchi hizo mbili zimekuwa katika msuguano kuhusu kiwango cha urutubishaji madini ya urani.

"Haiwezi kusemwa kwa vyovyote vile kwamba kila nchi inayojihusisha na kurutubisha urani lazima iwe na mpango wa silaha. Hivi sasa, nchi nyingi, ikiwa ni pamoja na baadhi ya washirika wa Marekani, zinajishughulisha na kurutubisha madini hayo lakini hazina mipango yoyote ya kijeshi au silaha," mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran amesema.

Amesisitiza kuwa, urutubishaji urani ni hitajio la kistratijia kwa sekta ya nyuklia ya Iran na kuhudumia maslahi ya taifa hili. "Teknolojia hii ya kiasili imestawishwa kupitia miongo kadhaa ya juhudi endelevu za wanasayansi wa Iran, na kwa vyovyote vile, sio mada iliyo wazi kwa majadiliano au maelewano."

Kuhusu duru ijayo ya mazungumzo ya nyuklia, Baghaei amesema, "Kwa wakati huu, sina chochote maalum cha kuwaeleza waandishi wa habari kuhusu duru ya sita ya mazungumzo; ikiwa uamuzi utafanywa, itatangazwa baadaye."

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa, pendekezo lolote lisilozingatia maslahi ya Iran halikubaliki, na kwamba Tehran hivi karibuni itawasilisha pendekezo lake kupitia Oman.