Iran: Tutapiga vituo vya siri vya nyuklia vya Israel iwapo tutashambuliwa
(last modified Tue, 10 Jun 2025 03:03:10 GMT )
Jun 10, 2025 03:03 UTC
  • Iran: Tutapiga vituo vya siri vya nyuklia vya Israel iwapo tutashambuliwa

Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran (SNSC) limeonya kuwa, Jamhuri ya Kiislamu itavishambulia vituo vya siri vya nyuklia vya Israel iwapo utawala huo wa Kizayuni utafanya kitendo chochote cha uchokozi dhidi ya taifa hili.

Katika taarifa yake, baraza hilo limesema kuwa, operesheni ngumu ya kiintelijensia ya majeshi ya Iran na mafanikio yao makubwa ni sehemu kuu ya mpango mahiri na vitendo vya siri vya mfumo mtukufu wa Kiislamu mbele ya propaganda za maadui.

Imeongeza kuwa, sehemu nyingine kuu ya mpango huo ni pamoja na juhudi zisizo na kikomo za Vikosi vya Ulinzi za kuleta mlingano wa nguvu kiutendaji, kulingana na udhaifu na nguvu za utawala ghasbu wa Israel na waungaji mkono wake.

Baraza hilo limesema orodha inayolengwa na Israel ipo juu ya “meza” ya Vikosi vya Jeshi la Iran, na kwamba vituo vya siri vya nyuklia vya utawala huo vitalengwa iwapo vitafanya chokochoko za aina yoyote.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, leo hii majeshi ya Iran yana uwezo wa "kujibu mara moja uchokozi wowote unaoweza kufanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya vituo vya nyuklia vya nchi hii, kwa kushambulia vituo vya siri vya nyuklia (vya Israel)."

Kituo cha nyuklia cha Israel cha Dimona

Kabla ya hapo, Esmail Khatib, Waziri wa Usalama wa Taifa wa Iran, alisema kuwa nyaraka za siri ambazo Iran imefanikiwa kuzipata kutoka Israel, zinahusiana moja kwa moja na taarifa nyeti kuhusu miundombinu ya nyuklia ya utawala huo ghasibu na zinaimarisha uwezo wa Iran kuhujumu.

Akizungumza na shirika la habari la IRIB siku ya Jumapili, siku moja baada ya vyanzo vya kuaminika kufichua habari hizo, Khatib amesema: "Nyaraka tulizopata kutoka utawala wa Kizayuni zinahusiana na taarifa kuhusu vituo vyao vya nyuklia." Amesema nyaraka hizo za siri, pamoja na taarifa nyingine za kimkakati, zitaboresha uwezo wa Iran wa kushambulia.