Qalibaf: Marekani ni lazima ilipe gharama za jinai za Israel Lebanon
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i138822-qalibaf_marekani_ni_lazima_ilipe_gharama_za_jinai_za_israel_lebanon
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) Mohammad Baqir Qalibaf ameilaani Marekani kwa kuhusika katika mashambulizi ya utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Lebanon na kueleza kuwa Washington lazima ilipe gharama ya jinai za kivita zinazofanywa na utawala huo ghasibu dhidi ya Lebanon.
(last modified 2026-06-02T03:07:39+00:00 )
Jun 02, 2026 03:01 UTC
  • Mohammad Baqir Qalibaf, Spika wa Bunge la Iran
    Mohammad Baqir Qalibaf, Spika wa Bunge la Iran

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) Mohammad Baqir Qalibaf ameilaani Marekani kwa kuhusika katika mashambulizi ya utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Lebanon na kueleza kuwa Washington lazima ilipe gharama ya jinai za kivita zinazofanywa na utawala huo ghasibu dhidi ya Lebanon.

Spika Qalibaf jana Jumatatu alituma ujumbe katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X zamani Twitter akiikosoa Marekani kwa kushindwa kufungamana na usitishaji vita. Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran ametaja mzingiro wa jeshi la majini la Israel na mashambulizi makali ya anga ya utawala huo dhidi ya Lebanon kuwa ni ushahidi wa wazi wa ukiukwaji wa sheria unaofanywa na Marekani.

"Mzingiro wa majini na kuongezeka jinai za kivita nchini Lebanon zinazofanywa na utawala wa Kizayuni unaotenda mauaji ya kimbari ni ushahidi wa wazi wa kutofungamana  Marekani na usitishaji vita," ameandika Spika Qalibaf katika akaunti yake ya X.

Televisheni ya al Jazeera ya Qatar imeripoti kuwa mashambulizi ya anga ya karibuni ya Israel yamesababisha maelfu ya wakazi wa kusini mwa Lebanon kuhama makazi yao na kuelekea maeneo salama ikiwa ni pamoja na eneo la Mlima Lebanon, katika miji ya kaskazini na baadhi ya maeneo ya mji mkuu Beirut.

Baadhi ya raia wa Lebanon wamesalia majumbani mwao licha ya kutolewa tahadhari za kuhama huku idadi ya majeruhi wa mashambulizi ya anga ya Israel ikiongezeka.

Mazungumzo kati ya Lebanon, Marekani na utawala wa Israel, yaliyofanyika Pentagon mwishoni mwa juma, yalivunjika baada ya saa tisa bila kufikia ufumbuzi wowote. Utawala wa Kizayuni wa Israel umekataa pendekezo la Lebanon ambayo ilitaka wanajeshi wa Israel waondoke nchini humo huku Rais wa Lebanon akisema kuwa yupo tayari kwa mazungumzo mapya.

Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, Marekani na utawala ghasibu wa Israel zinapanga njama ya kuishinikiza Lebanon ili kuipokonya silaha Harakati ya Muqawama ya Hizbullah kupitia makubaliano ya usalama.