Kwa nini Trump anatapatapa kati ya vitisho na makubaliano?
CNN imesema katika ripoti kwamba: "Serikali ya Marekani huchanganyikiwa linapokuja suala la nyuklia la Iran." Katika kipindi cha wiki kadhaa zilizopita, Rais Donald Trump wa Marekani amebadilisha misimamo yake mara kadhaa kuhusu hatima ya hifadhi ya urani iliyorutubishwa ya Iran.
Siku moja anadai kuwa "haina maana" na kusema ufuatiliaji wa satelaiti unatosha; ya pili anazungumzia kuihamishia Marekani, muda mfupi baadaye anaashiria fikra ya kuzika na kuifungia, na hatimaye anasisitiza juu ya kuiharibu au kuiondoa nchini Iran. Migongano hii ya wazi haipaswi kubanwa tu katika shakhsia isiyotabirika ya Trump. Kuchanganyikiwa huku kwa Washington, kabla ya jambo lolote lile, kunaakisi taswira ya mkwamo wa kimkakati wa Marekani baada ya vita vyake vya kichokozi vya siku arubaini dhidi ya Iran. Vita ambavyo, kinyume na mahesabu ya awali ya White House na Tel Aviv, havikupelekea kusambaratika kwa nguvu ya kijeshi ya Iran, kuvuruga miundo ya kistratijia ya Jamhuri ya Kiislamu, wala kuilazimisha Tehran ikubali masharti ya kibabe ya Marekani.
Trump na watu wanaomzunguka walidhani kuwa licha ya kushindwa kufikia malengo yao makuu ya uvamizi wa kijeshi dhidi ya Iran, wangeweza, kupitia mseto wa mashinikizo ya kijeshi, kiuchumi na kisaikolojia, kuiweka Iran katika hali ambayo ingeibana na kuilazimisha ikubali masharti yao ya kijuba ili kumaliza mgogoro uliopo, ikiwa ni pamoja na kukubali vikwazo vikali vya nyuklia, kufuta mpango wake wa makombora, na hata kufafanua upya nafasi yake katika eneo. Pamoja na hayo lakini kile kilichotokea ni tofauti kabisa na matarajio hayo. Si tu kwamba Iran imeweza kudumisha uwezo wa kijeshi na miundombinu yake, bali kwa kulenga vituo vya Marekani katika eneo na kudumisha mshikamano wa ndani, imetuma ujumbe wa wazi kwamba gharama ya vita vyovyote vile itazidi makadirio ya awali ya Washington. Trump sasa anakabiliwa na hali ya kukatisha tamaa. Anahitaji kubuni "mafanikio" ya kisiasa kwa sababu rais ambaye alianzisha vita kwa kauli mbiu ya kuishinda haraka Iran sasa analazimika kuthibitisha na kuwaonyesha hadharani Wamarekani na washirika wake wa kieneo, mafanikio hayo.
Suala la urani iliyorutubishwa ya Iran limegauka kuwa nembo muhimu katika muktadha huo. Nembo ambayo Ikulu ya Marekani inajaribu kuiwasilisha kama "fursa iliyopokonywa Iran." Lakini hali halisi ya mambo kwenye medani na masuala ya kiufundi yameifunga mikono ya Trump. Baada ya miaka mingi ya vikwazo, mauaji ya kigaidi dhidi ya wanasayansi wa nyuklia, wasomi na viongozi wa kisiasa, vitendo vya uharibifu na mashinikizo ya kisiasa, Iran sio tu imehifadhi teknolojia yake ya nyuklia, bali pia imeweza kuimarisha mzunguko wa teknolojia hiyo ndani ya nchi. Hata kama tutafaradhisha kwamba sehemu ya hifadhi yake ya urani itahamishiwa nje ya nchi au kubanwa kabisa, lakini bado ujuzi wa kiufundi, miundombinu ya rasilimali watu na uwezo wa kukarabati haraka mpango wa nyuklia vitaendelea kuwepo nchini.
Hili limezifanya baadhi ya taasisi za usalama za Marekani kuwa na wasiwasi na mbinu hizo za kipropaganda. Misimamo inayogongana ya Trump kuhusu hatima ya urani iliyorutubishwa ya Iran pia inatokana na hali hii ya kukata tamaa. Anaposema kuwa "urani hii haina umuhimu wowote," kwa hakika anaashiria ukweli wa kiufundi. Kuwa na akiba ya urani hakumaanishi uwezo wa kutengeneza haraka silaha za nyuklia, kwa sababu habari za kiusalama na satelaiti zinaweza kufuatilia kwa karibu shughuli zinazofanyika katika uwanja huo. Lakini anapozungumzia kuhamishwa au kuharibiwa hifadhi ya urani, anajibu hitajio lake la kisiasa la angalau kuonyesha ushindi wa kimaonyesho dhidi ya Iran.
Mgongano huu unathibitisha wazi kuwepo hitilafu ndani ya serikali ya Marekani. Baadhi ya timu ya Trump, ikiwa ni pamoja na maafisa kama vile Marco Rubio Waziri wa Mambo ya Nje na Scott Besant, Waziri wa Fedha wanaendelea kusisitiza juu ya sera ya mashinikizo na kupata fursa zaidi kutoka kwa Iran. Wanaamini kwamba kutohamishwa akiba ya urani kutoka Iran kutakuwa na maana ya kushindwa kwingine kwa Marekani baada ya vita. Lakini katika upande wa pili, kuna mrengo unaozingatia zaidi uhalisia wa mambo unaoona kwamba baada ya vita, Iran sio Iran ya kabla ya vita na kwamba Tehran haiko katika nafasi dhaifu ya kukubali masharti yanayotolewa na Marekani. Muhimu zaidi ni kuwa, Marekani sasa inakabiliwa na changamoto za kijiopolitiki. Washington inakabiliwa na mashindano ya wakati mmoja ya China na Russia na haina uwezo wa kuingia katika mzozo mpya wa kuchosha Asia Magharibi. Mbali na hayo, uzoefu mchungu wa Iraq na Afghanistan bado ni mpya katika kumbukumbu ya kimkakati ya Marekani. Jaribio lolote la kuzidisha mzozo na Iran linaweza kuisababishia Marekani na washirika wake gharama zisizotabirika za kiuchumi na kiusalama. Kwa kuzingatia ukweli huu, kile ambacho CNN inakiita "kuchanganyikiwa" kwa kweli ni dalili ya tatizo kubwa zaidi ambalo ni Washington kutokuwa na uwezo wa kubadilisha ubabe wake wa kijeshi kuwa faida ya kisiasa. Baada ya vita vya siku arubaini, Trump ameshindwa kuilazimisha Iran irudi nyuma kimkakati, wala hajaweza kuwasilisha mfumo wa wazi wa makubaliano na Iran baada ya vita. Sasa amenasa kati ya chaguzi mbili kuu: ima kufikia makubaliano halisi ambayo yanaweza kuwa chini ya matarajio ya awali ya Marekani, au kuendeleza mashinikizo ambayo yanaweza kupelekea kushindwa kwingine kidiplomasia.
Kwa mtazamo huu, kichanganyikiwa Trump juu ya suala la nyuklia la Iran hakutokani na mvurugiko wa kisiasa, bali ni dhihirisho la pengo kubwa lililopo kati ya matarajio ya kijiopolitiki ya Marekani na ukweli halisi wa nguvu ya Iran uwanjani. Washington bado inataka kufikia makubaliano ambayo itayachukulia kama "ushindi," lakini ukweli wa mambo ni kwamba baada ya vita, Iran imethibitisha wazi kuliko wakati mwingine wowote kwamba haiko tayari kubadilishana na hasimu wake, usalama na uwezo wake wa kimkakati na makubaliano yasiyo endelevu na dhaifu.