Ni jinai gani nyingine imebakia haijafanywa na Israel
(last modified Fri, 30 May 2025 03:03:20 GMT )
May 30, 2025 03:03 UTC
  • Ni jinai gani nyingine imebakia haijafanywa na Israel

Maafa ya kibinadamu huko Ghaza Palestina yamefika kileleni kiasi kwamba katika uhalifu wa karibuni zaidi wa Israel, jeshi katili la utawala wa Kizeyuni limeshambulia vituo vya usambazaji chakula ambavyo Israel yenyewe ilikubali viwepo na mpaka iliainisha viwekwe maeneo gani.

Duru za habari zimeripoti kuwa, jana jioni ulisikika mripuko mkubwa karibu na kituo cha usambazaji misaada kwenye eneo la Netzarim, katikati mwa Ukanda wa Ghaza.

Baada ya hapo, vyombo vya habari vya Palestina viliripoti kufanyika shambulio kubwa la Israel na kusababisha maafa yasiyoelezeka kwa Wapalestina waliokwenda eneo hilo kupokea misaada ya kibinadamu.

Kabla ya kutangaza habari hiyo tayari Wizara ya Afya ya Palestina huko Ghaza ilikuwa imetangaza kuwa katika muda wa saa 48 zilizopita, watu 9 walikuwa wameuawa shahidi na zaidi ya 60 kujeruhiwa wakati wa shambulio jingine la kikatili lililofanywa na jeshi la Israel karibu na vituo vya kusambaza misaada vinavyoendeshwa na kampuni moja ya Kimarekani huko Rafah.

Baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii walisambaza picha ya mmoja wa majeruhi wa uhalifu huu na jinsi alivyosafirishwa hadi mahali kwa matibabu, wakiandika: "Hivi ndivyo mtu aliyejeruhiwa kwa risasi na jeshi la Israel akipelekwa kituo cha matibabu na hii ndiyo hali ya Ghaza."

Maelezo mengine yamesema: "Mtu huyu alikuwa anajaribu kufika kwenye kituo cha 'misaada' cha Marekani kilichoko kati ya Rafah na Khan Yunis. Maeneo haya si vituo vya kusambaza misaada, bali ni maeneo yaliyotengwa na Marekani ili Israel ipate kuua na kuangamiza vijana wa Kipalestina.”