Sababu za kuendelea Muqawama wa Yemen licha ya uungaji mkono mkubwa wa Marekani na Magharibi kwa utawala wa Kizayuni
Licha ya uungaji mkono mkubwa wa Marekani na nchi za Magharibi kwa utawala ghasibu wa Israel, lakini operesheni za wapiganaji wa muqawama wa Yemen katika Bahari Nyekundu na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu zingali zinaendelea.
Jeshi la Yemen limekuwa likilenga mara kwa mara maeneo ya ndani kabisa ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel. Duru za habari zimeripoti milipuko kadhaa iliyotokea katika siku za karibuni katikati ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu na vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kufuatia kombora lililorushwa kutokea Yemen.
Mike Huckabee, balozi wa Marekani katika utawala wa Kizayuni amekiri kuwepo hali ya mgogoro katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kufuatia mashambulizi ya makombora kutoka Yemen na kusema: "mara nyingi tunalazimika kukimbilia kwenye maficho yaliyoko chini ya ardhi kwa kuhofia mashambulizi ya makombora ya Yemen. Tunaposikia ving'ora, inabidi tuhame ubalozi na kuwapeleka wafanyakazi wote kwenye maficho hayo ya chini ya ardhi."
Brigedia Jenerali Yahya Saree, msemaji wa jeshi la Yemen ametangaza katika taarifa kwamba, jeshi la nchi hiyo, ikiwa ni katika kuwasaidia wananchi na wapiganaji wa Palestina katika kukabiliana na mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni huko Gaza, limelenga uwanja wa ndege wa Tel Aviv's, Ben Gurion kwa makombora mawili ya balistiki.
Msemaji huyo wa jeshi la Yemen ameongeza kuwa: "Shambulio hilo limetekelezwa kwa makombora mawili ya balistiki, moja likiwa limepiga moja kwa moja uwanja huo wa ndege, ambapo mifumo ya ulinzi ya utawala wa Israel ilishindwa kukabiliana nayo."
Mahdi Al-Mashat, Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen pia amesisitiza kuwa: "Majibu kwa hujuma yoyote ya utawala wa Kizayuni dhidi ya ardhi ya Yemen yamezingatiwa na yatakuwa ya pande kadhaa."
Katika kujaribu kuvunja mzingiro wa jeshi la majini na anga la jeshi la muqawama la Yemen, utawala wa Kizayuni umefanya mashambulizi kadhaa dhidi ya raia wa Yemen na kusababisha makumi ya mashahidi na majeruhi. Licha ya mashambulizi hayo, jeshi la Yemen linaendelea kuunga mkono muqawama na wananchi wa Palestina huko Gaza, ambapo limefanya operesheni za kipekee zikilenga maeneo ya ndani na meli za utawala wa Kizayuni katika Bahari Nyekundu na Bahari ya Hindi.

Mafanikio ya operesheni za majeshi ya muqawama ya Yemen katika kukabiliana na muungano wa Marekani, Magharibi na Wazayuni yanatokana na mambo mbalimbali ya kistratijia, kijeshi, kijiografia na kiitikadi.
Vikosi vya muqawama vya Yemen vinatumia makombora ya hali ya juu na ndege zisizo na rubani ambazo zina uwezo wa kukwepa mifumo ya ulinzi ya ngome ya Iron Dome ya Israel. Vikosi hivyo vimewashtua wanajeshi wa Marekani kwa kutumia mbinu na silaha za hali ya juu kama vile makombora ya kisasa katika kulenga manowari za Marekani katika Bahari Nyekundu.
Kwa kuwa na maeneo mengi ya milimani, kama vile Saada na kupakana na Bahari Nyekundu, vikosi vya jeshi la Yemeni vina uwezo mkubwa wa kupeleka silaha katika maeneo hayo salama na kufanya mashambulizi ya kushtukiza dhidi ya adui. Bandari ya Hodeidah, kama eneo la kimkakati, imewawezesha Wayemen kudhibiti vizuri usafiri wa baharini. Muqawama wa Yemen umeimarisha miundombinu ya kutengeneza silaha na kuiweka salama dhidi ya mashambulizi ya adui.
Suala jingine muhimu ni mfungamano wa mapambano ya vikosi vya muqawama wa Yemen na kadhia ya Palestina, jambo ambalo limevutia uungaji mkono wa ndani na kieneo. Muqawama wa Yemen unachukulia operesheni zake kama "wajibu wa kidini na wa kibinadamu" ambao unaimarisha ari ya vikosi na wafuasi wake.
Marekani na utawala haramu wa Israel wameshindwa kabisa kusimamisha mashambulizi ya Yemen. Ripoti zinaonyesha kuwa mashambulizi ya Marekani licha ya kuigharimu zaidi ya dola bilioni 1 tangu Machi 2025, lakini yamekuwa na taathira ndogo sana kwa uwezo wa muqawama wa Yemen.
Mchanganyiko wa "ubunifu wa kijeshi", "eneo la kijiografia", "uungaji mkono wa wananchi" na "makosa ya adui" umeviwezesha vikosi vya muqawama vya Yemen kustahimili mashambulizi ya Marekani na utawala wa Kizayuni na kuwa nembo ya kuzuia hujuma za adui katika eneo. Mafanikio haya pia yanaonyesha kuwa vita visivyo na uwiano wa kijeshi vinaweza kuyaibulia changamoto kubwa majeshi makubwa na yanayoendeshwa kwa gharama kubwa duniani kama vile ya Marekani.
Umuhimu na taathira za operesheni za jeshi la Yemen katika kulenga nukta muhimu za kijeshi na kijasusi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu ni kwamba zimeharibu pakubwa miundo ya usalama ya utawala wa Kizayuni. Ubora wa kijeshi wa Yemen katika Bahari Nyekundu umewapelekea watawala wa Marekani kukiri kuwa hawana uwezo wa kukabiliana na vikosi vya muqawama wa Yemen.