Njaa yashadidi Ukanda wa Gaza huku Israel ikiendelea kuzuia misaada
Ofisi ya Habari ya Serikali katika Ukanda wa Gaza imezitaka nchi zote duniani kuvunja mara moja mzingiro dhidi ya Gaza, kufungua mipaka kwa njia ya kudumu, na kuingiza misaada ya dharura , hasa unga na maziwa ya watoto wachanga, kwa ajili ya watu zaidi ya milioni 2.4 walioko chini ya mzingiro mkali ambao unatekelezwa na utawala katili wa Israel.
Taarifa hiyo imethibitisha kuwa kufikia saa 9:00 alasiri siku ya Alhamisi, hakuna hata lori moja la misaada lililoruhusiwa kuingia Gaza, hali inayoashiria kuwa njaa inazidi kuwa mbaya, hatari, na kusambaa kwa kasi katika maeneo yote ya Ukanda huo.
Ofisi hiyo imeeleza kuwa hali hii imetokea kufuatia kufungwa kabisa kwa mipaka yote na jeshi la Israel kwa siku 145 mfululizo, pamoja na kuzuia kwa makusudi kuingia kwa maziwa ya watoto wachanga na misaada mingine ya kibinadamu.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Gaza inahitaji kwa haraka zaidi ya magunia 500,000 ya unga ngano kila wiki ili kuepusha janga kamili la kibinadamu.
Pia, imetoa wito kwa vyombo vya habari na waandishi habari kuhakikisha uandishi wa habari sahihi na kutumia vyanzo rasmi ili kuonyesha hali halisi inayoendelea Gaza.
Wakati huo huo, maandamano yameibuka katika maeneo mbalimbali duniani kulaani mzingiro wa kibinadamu unaowekwa na Israel dhidi ya Gaza, ambapo raia wa Palestina wanapoteza maisha kutokana na mashambulizi ya kijeshi au njaa inayosababishwa na ukosefu wa bidhaa muhimu.
Maandamano yameripotiwa katika miji kadhaa ya Ulaya, katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na hata ndani ya Israel, huku waandamanaji wakiulaani vikali utawala wa Tel Aviv kwa kutumia njaa kama silaha ya dhidi ya Wapalestina ili kuwashinikiza wasalimu amri na waondoke katika ardhi yao ya jadi.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN), baa la njaa linatishia maisha ya mamia ya maelfu ya raia wa Gaza, hususan watoto. Picha za kusikitisha za utapiamlo zimekuwa zikienea kila siku.
Wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu, raia na familia zao wote wanatoa wito wa kusitishwa kwa mzingiro huo mara moja na kutoa fursa ya kuwasilisha chakula na huduma za matibabu kwa haraka.
Ikumbukwe kuwa Israel ilianzisha mashambulizi yake ya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza mnamo Oktoba 7, 2023. Tangu wakati huo, zaidi ya Wapalestina zaidi ya 59, 000 wameuawa shahidi, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto, kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza.
3493970