Haaretz: Israel iliua watoto 1,000 wa Kipalestina mwezi uliopita
Gazeti la Kizayuni la "Haaretz" limekiri Jumamosi ya leo kwamba, jeshi la utawala huo liliua watoto 1,000 katika mashambulizi yake katika Ukanda wa Gaza mwezi uliopita pekee.
Gazeti la Haaretz limeandika katika toleo lake la leo Jumamosi: Jeshi la Israel liliua takriban watoto elfu moja katika Ukanda wa Gaza mwezi uliopita wa Juni. Masaa machache yaliyopita, vyanzo vya habari viliripoti kwamba idadi ya mashahidi waliokufa kwa sababu ya njaa huko Gaza imeongezeka na kufikia Wapalestina 122, 83 kati yao ni watoto.
Kwa upande mwingine, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alisema katika hotuba yake kwa njia ya video katika Baraza Kuu la Amnesty International kwamba hakuna kinachoweza kuhalalisha milipuko, vifo na uharibifu huko Gaza tangu vita hivyo vilipoanza.
Takwimu za hivi karibuni zilizotolewa na Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa karibu watu nusu milioni wanakabiliwa na viwango vya juu kabisa vya njaa. Mashirika ya misaada yameripoti kuwa zaidi ya Wapalestina 100, watoto wakiwa ndio waathirika wakuu, wamefariki dunia kwa njaa katika wiki chache zilizopita, huku hospitali zikishindwa kutoa huduma kwa maelfu ya watoto waliokonda kupita kiasi.
Ufikishaji wa misaada ya kibinadamu bado unakumbwa na vikwazo vikubwa, kutokana na hatua za kijeshi za Israel zinazozuia au kushambulia misafara ya misaada inayojaribu kufika Gaza ya kaskazini na kati. Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) pamoja na mashirika mbalimbali ya kimataifa wameeleza kuwa hali hiyo ni baa la njaa lililotengenezwa kwa makusudi na wameitaka jumuiya ya kimataifa kuiwekea Israel mashinikizo ya moja kwa moja ili kuondoa mzingiro mara moja.