Chama cha Soka Palestina: Wanasoka 355 wameuawa shahidi na Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i130042-chama_cha_soka_palestina_wanasoka_355_wameuawa_shahidi_na_israel
Mkuu wa Shirikisho la Soka la Palestina amekosoa uzembe wa Shirikisho la Soka Duniani FIFA na taasisi za kimataifa na kutaka kuchukuliwa hatua za haraka dhidi ya hujuma za utawala wa Kizayuni dhidi ya michezo Palestina.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Aug 27, 2025 00:46 UTC
  • Chama cha Soka Palestina: Wanasoka 355 wameuawa shahidi na Israel

Mkuu wa Shirikisho la Soka la Palestina amekosoa uzembe wa Shirikisho la Soka Duniani FIFA na taasisi za kimataifa na kutaka kuchukuliwa hatua za haraka dhidi ya hujuma za utawala wa Kizayuni dhidi ya michezo Palestina.

Jibril Rajoub, Mkuu wa Shirikisho la Soka la Palestina ametoa wito kwa FIFA, Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki na taasisi zote za michezo duniani kuacha "kukwepa majukumu" na kuchukua maamuzi madhubuti ya kukomesha hujuma za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya sekta ya michezo ya Palestina.

Amesisitiza kuwa jamii ya kimataifa ya michezo haitakiwi kukaa kimya mbele ya jinai hizo na lazima itimize wajibu wake wa kisheria na kimaadili.

Mkuu wa Shirikisho la Soka la Palestina amesema: "FIFA imeshindwa kushughulikia kile kinachotokea kwa michezo ya Palestina na, badala ya kutekeleza sheria, inafanya kazi kindumakuwili. Tabia hii haikubaliki kwa chombo cha kimataifa ambacho kazi yake ni kuzingatia sheria na kanuni zake."

Jibril Rajoub, Mkuu wa Shirikisho la Soka la Palestina

 

Katikka mkutano wake na waandishi wa habari Rajoub kisha ameonyesha video ya uharibifu na maafa yaliyosababishwa dhidi ya sekta ya michezo ya Palestina tangu Oktoba 7, 2023, ambapo akielezea ukubwa wa janga hili amesema kwamba, michezo ya Palestina inakabiliwa na "mgogoro wa kibinadamu ambao haujawahi kutokea katika historia ya sasa."

Aidha akitoa takwimu kamili za hasara hizi alisema: Hadi sasa kuna mashahidi 774 kutoka miongoni mwa jamii ya wanamichezo, ikiwa ni pamoja na wachezaji wa mpira wa miguu 355, wanachama 277 wa mashirikisho ya michezo, 142 kutoka Harakati ya Skauti ya Palestina na 15 kutoka Muungano wa Vyombo vya Habari vya Michezo. Pia, wanariadha 119 wametoweka na viwanja 288 vya michezo katika Ukingo wa Magharibi na Gaza vimeharibiwa kabisa au kwa sehemu fulani. Kulingana na Rajoub, baadhi ya maeneo haya, kama vile Uwanja wa Palestina na Yarmouk, yamekuwa makazi ya watu waliokimbia makazi yao.