Rais wa Lebanon aiomba Marekani kuishinikiza Israel iondoke kusini mwa Lebanon
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i130518-rais_wa_lebanon_aiomba_marekani_kuishinikiza_israel_iondoke_kusini_mwa_lebanon
Rais wa Lebanon, Joseph Aoun, ameitaka Washington kuishinikiza Israel ili ikomeshe kukalia kwa mabavu ardhi ya kusini mwa nchi hiyo, akisema hatua hiyo itafungua njia kwa jeshi la Lebanon kuchukua udhibiti kamili wa eneo hilo.
(last modified 2025-09-07T08:28:57+00:00 )
Sep 07, 2025 08:28 UTC
  • Joseph Aoun
    Joseph Aoun

Rais wa Lebanon, Joseph Aoun, ameitaka Washington kuishinikiza Israel ili ikomeshe kukalia kwa mabavu ardhi ya kusini mwa nchi hiyo, akisema hatua hiyo itafungua njia kwa jeshi la Lebanon kuchukua udhibiti kamili wa eneo hilo.

Wito huo ulitolewa jana Jumamosi wakati wa mkutano wa Aoun na Admiral Brad Cooper, kamanda wa Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM), uliofanyika mjini Beirut.

Shirika la Habari la Taifa la Lebanon (NNA) limeripoti kuwa, Aoun aliitaka Marekani kuishinikiza Israel itekeleze makubaliano ya kusitisha mapigano ya Novemba 2024, kukomesha operesheni zake za kijeshi dhidi ya Lebanon, kuondoka katika vituo vitano vinavyokaliwa kwa mabavu kusini mwa nchi hiyo, na kuwaachilia watu waliotekwa nyara wa Lebanon.

"Mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Israel kusini yanazuia kupelekwa jeshi la Lebanon kwenye mpaka," Aoun alisema na kuongeza kuwa, vikosi vya jeshi tayari vimewekwa katika zaidi ya asilimia 85 ya eneo la kusini mwa Mto Litani.

Vita viwili vilivyoanzishwa na Israel dhidi ya Lebanon mwaka 2000 na 2006 vilikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa harakati ya Hizbullah ambayo ilililazimisha jeshi la utawala huo kurudi nyuma.

Mwaka 2006, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha kwa kauli moja Azimio nambari 1701, ambalo lilimaliza vita kati ya Hizbullah na Israel.

Azimio hilo lilitaka kusitishwa mapigano kwa kudumu na kuanzishwa eneo la ukanda unaotenganisha pande mbili kusini mwa Lebanon.