Save the Children: Kila saa moja mtoto mmoja anauawa shahidi Gaza
Shirika la Kimataifa la Save the Children limetangaza kuwa, hali ya watoto Gaza ni mbaya mno na kwamba, kila saa moja mtoto mmoja anauawa shahidi katika Ukanda huo unaokabiliwa na mzingiro.
Hayo yamo katika ripoti iliyotolewa na Shirika la Kimataifa la "Save the Children" ambayo imebainisha kuwa, mtoto mmoja anauawa shahidi kila saa katika Ukanda wa Gaza, na kwamba, zaidi ya watoto 20,000 wa Kipalestina wameuawa na wengine 21,000 wamepata ulemavu wa kudumu katika hujuma za kijeshi za Israel dhidi ya eneo hilo.
Kwa mujibu wa mtandao wa Al-Mayadeen, shirika la kimataifa la "Save the Children" limesema katika ripoti yake kwamba, idadi ya watoto waliouawa shahidi katika Ukanda wa Gaza katika kipindi cha karibu miezi 23 ya vita vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wanawake na watoto katika eneo hilo imezidi 20,000, jambo ambalo lina maana kwamba, kwa uchache mtoto mmoja wa Kipalestina amepoteza maisha kila saa.
Likinukuu data za hivi punde kutoka kwa ofisi ya habari ya serikali ya Palestina katika Ukanda wa Gaza, shirika hilo liliripoti kwamba angalau watoto 20,000, au karibu asilimia 2 ya watoto wote katika Ukanda wa Gaza, wameuawa shahidi tangu Oktoba 2023.
Ripoti ya shirika hili pia inaonyesha kuwa takriban watoto 1,09 walio chini ya umri wa mwaka mmoja wameuawa shahidi, huku karibu nusu ya watoto hao (450) wakizaliwa na kuuawa wakati wa vita.
Pia, kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Gaza, kwa uchache watoto 42,011 wamejeruhiwa wakati wa vita. Kadhalika, Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Watu wenye Ulemavu umetangaza kuwa, angalau watoto 21,000 wa Kipalestina wamepata ulemavu wa kudumu, wakati maelfu ya wengine bado hawajulikani au wanaaminika kuzikwa chini ya vifusi.