Israel yafanya shambulio la kigaidi Qatar na kulenga ujumbe wa Hamas
Shambulio la kigaidi lililotekelezwa na utawala ghasibu wa Israel huko Doha mji mkuu wa Qatar limelenga maeneo ya makazi yanayohusishwa na wajumbe wa ngazi ya juu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS.
Habari hizo zimekuja baada ya milipuko kadhaa kuripotiwa katika mji mkuu, Doha, leo Jumanne, huku moshi ukiongezeka kutoka wilaya ya Katara.
Chanzo kikuu cha Hamas kiliiambia Al Jazeera: Ujumbe wa mazungumzo ya Hamas ulilengwa wakati wa mkutano wake huko Doha.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran, Ismail Baqaei amelaani mashambulizi hhayo ya utawala wa kizayuni dhidi ya Qatar na dhidi ya ujumbe wa Hamas na kuyataja kuwa ni hatari kubwa na ukiukaji wa kanuni, malengo na kanuni zilizoainishwa katika Hati ya Umoja wa Mataifa.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar imelaani "shambulio la kigaidi" la Israel huko Doha.
Hadi sasa hakuna taarifa za kuaminika kuhusiana na hatima ya ujumbe na viongozi wa Hamas waliolengwa katika shambulio hilo la kigaidi ingawa baadhi ya duru zinasema kuwa, viongozi hao wa HAMAS wamenusurika kifo.
Qatar, mpatanishi mkuu wa kikanda katika mazungumzo yanayoendelea ya kusitisha mapigano Gaza. Ripoti za milipuko katikati ya Doha zinaweza kuibua wasiwasi wa kikanda, ingawa maelezo ya kina zaidi kuhusiana na shambulio hilo la kigaidi bado hayajatolewa.
Baadhi ya duruu zimeinukuu Israel ikisema kuwa mashambulizi hayo yametekelezwa kwa ushirikiano na Marekani.
Ujumbe huo wa HAMAS ulikuwa umejumuika kujadili mapendekezo ya Marekani ya kusitisha mauaji ya halaiki yanayotekelezwa na utawala wa Kizayuni huko katika Ukanda wa Gaza.