Israel yaua waandishi habari 24 wa Yemen ikijaribu kunyamazisha sauti ya haki
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i130784-israel_yaua_waandishi_habari_24_wa_yemen_ikijaribu_kunyamazisha_sauti_ya_haki
Katika kile kinachoonekana kama kuongezeka kwa kampeni ya kigaidi ya wazi na ya kunyamazisha sauti ya haki, utawala haramu wa Israel umetekeleza mojawapo ya mashambulio mabaya zaidi dhidi ya waandishi wa habari katika historia ya kisasa, kwa kuwalenga na kuwaua angalau waandishi 25 wa habari wa Yemen mjini Sana’a.
(last modified 2025-09-14T03:33:50+00:00 )
Sep 14, 2025 03:33 UTC
  • Israel yaua waandishi habari 24 wa Yemen ikijaribu kunyamazisha sauti ya haki

Katika kile kinachoonekana kama kuongezeka kwa kampeni ya kigaidi ya wazi na ya kunyamazisha sauti ya haki, utawala haramu wa Israel umetekeleza mojawapo ya mashambulio mabaya zaidi dhidi ya waandishi wa habari katika historia ya kisasa, kwa kuwalenga na kuwaua angalau waandishi 25 wa habari wa Yemen mjini Sana’a.

Shambulio hilo la Jumatano, ambalo liliharibu ofisi za magazeti ya Al-Yaman na 26 September, linachukuliwa kama hujuma ya moja kwa moja dhidi ya vyombo vya habari katika eneo hili, na linahesabiwa kuwa uhalifu mkubwa wa kivita.

Ni tukio la kikatili zaidi dhidi ya waandishi wa habari kuwahi kurekodiwa tangu Novemba 2009, wakati waandishi 32 wa habari waliuawa katika maangamizi ya Maguindanao huko Ufilipino.

Kwa jumla, watu 58 waliuawa katika shambulio hilo la Israel dhidi ya waandishi habari Sanaa  na kulifanya kuwa tukio la kikatili zaidi dhidi ya waandishi wa habari duniani.

Katika Ukanda wa Gaza, utawala haramu wa Israel umeua zaidi ya waandishi habari 250 tangu Oktoba 2023, katika kile kinachotajwa kama jaribio la kimakusudi la kubana ripoti za waandishi habari wanaoandika kuhusu jinai za Israel.

Yemen, taifa lililojitokeza wazi kuunga mkono watu wa Palestina wanaokumbwa na mauaji ya kikatili, sasa lenyewe limekuwa mhanga wa mashine ya mauaji ya Wazayuni.

Shirikisho la Waandishi wa Habari la Yemen, kupitia taarifa rasmi, limelaani vikali kulengwa kwa mashirika ya habari.

Wataalamu wa haki za binadamu wamelitaja tukio hilo kama mwendelezo wa sera ya makusudi ya Israeli ya kuwalenga waandishi wa habari, sera ambayo imeshadidishwa wakati wa kampeni ya kimbari dhidi ya Gaza.

Jaribio la jeshi la Israel la kutetea shambulio hilo kwa kudai kuwa ofisi za vyombo vya habari zilikuwa "makao ya uhusiano wa umma wa kijeshi" limetajwa kama uongo wa wazi, unaoakisi mkakati wa muda mrefu wa kuficha mashambulio dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari kupitia upotoshaji wa taarifa.

Waandishi wa habari wa Yemen wametoa wito kwa Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu kulaani uhalifu huu wa kivita, kuanzisha uchunguzi huru wa kimataifa, kuwawajibisha wahusika na kukomesha sera ya Israel ya kutowajibika ambayo inaongeza mashambulizi dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari.