Hamas yalaani mkutano wa 'Bodi ya Amani' ya Trump
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas imelaani vikali kufanyika mkutano wa kile kinachoitwa 'Bodi ya Amani ya Gaza' huko nchini Marekani.
Katika taarifa iliyotolewa Alkhamisi, Hamas imeeleza kwamba njia au mipango yoyote ya kisiasa kuhusu Gaza lazima itegemee kusitishwa kabisa kwa uchokozi na mashambulizi ya utawala haramu wa Israel dhidi ya wakazi wa ukanda huo.
Harakati hiyo ya Muqawama pia imesisitiza hitaji la kuondoa mzingiro dhidi ya Gaza na kuwadhaminia Wapalestina haki zao, ukiwemo uhuru na kujitawala na kujiamulia mustakabali wao.
Hamas imekosoa kufanyika mkutano huo nchini Marekani katika hali ambayo, utawala katili wa Israel unaendelea kufanya uhalifu katika eneo lililokumbwa na vita. Kadhalika Hamas imeonya kwamba, juhudi zozote za kweli za kimataifa za kuleta utulivu huko Gaza lazima zishughulikie chanzo cha matatizo; ambao ni ukaliaji wa mabavu wa Israel katika eneo hilo la Palestina—na kuwawezesha Wapalestina kupata haki zao za msingi.
Harakati hiyo ya Muqawama imewataka wapatanishi kuhakikisha makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza yanatekelezwa, na kuizuia Israel kukanyaga makubaliano hayo.
Wakati huo huo, harakati hiyo ya Kiislamu ya kupigania ukombozi wa Palestina katika Ukanda wa Gaza imesisitiza kuwa, makundi ya Palestina yamejitolea kuheshimu makubaliano hayo ya kusitisha mapigano, na kwamba mafanikio ya mapatano hayo sasa yanategemea kulazimishwa utawala haramu wa Israel kuyazingatia na kujiepusha na jinai inazoendeleza dhidi ya Wapalestina.
Ofisi ya Habari ya Gaza ilitangaza karibuni kwamba, tangu makubaliano ya kusitisha mapigano kuanza kutekelezwa mwanzoni mwa Oktoba mwaka jana, mashambulizi ya Israel yameua shahidi Wapalestina karibu 600 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 1,600. Aidha utawala huo wa Kizayuni umekiuka mapatano hayo zaidi ya mara 1,450.