Waziri wa kizayuni aeleza 'anavyofurahishwa' na mateso wanayopata wafungwa Wapalestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i141082-waziri_wa_kizayuni_aeleza_'anavyofurahishwa'_na_mateso_wanayopata_wafungwa_wapalestina
Waziri wa usalama wa ndani wa utawala wa kizayuni wa Israel, Itamar Ben-Gvir, amesema "anafurahishwa" na unyanyasaji wa wafungwa Wapalestina walioko kwenye jela za utawala huo na kuongeza kwamba yeye anahusika moja kwa moja na hali zinazoshuhudiwa katika jela hizo.
(last modified 2026-08-30T13:31:59+00:00 )
Aug 30, 2026 13:28 UTC
  • Waziri wa kizayuni aeleza 'anavyofurahishwa' na mateso wanayopata wafungwa Wapalestina

Waziri wa usalama wa ndani wa utawala wa kizayuni wa Israel, Itamar Ben-Gvir, amesema "anafurahishwa" na unyanyasaji wa wafungwa Wapalestina walioko kwenye jela za utawala huo na kuongeza kwamba yeye anahusika moja kwa moja na hali zinazoshuhudiwa katika jela hizo.

Ben-Gvir ametoa matamshi hayo baada ya video kusambaa kwenye mtandao wa kijamii wa Marekani wa X unaomuonyesha akizungumza na wafungwa wanawake wa Kipalestina.

"Hali hapa ni mbaya sana, na sisi wanawake hatupewi haki zozote maalumu kama vile kupata mahitaji yetu ya binafsi," anasikika mfungwa mmoja wa Kipalestina akizungumza katika video hiyo.

"Hii ni siku yetu ya tatu bila kuoga. Hatupati huduma za matibabu, na nguo zetu si safi," ameendelea kueleza mfungwa huyo mwanamke.

"Hali nzuri zilizozoeleka kuwepo magerezani hazipo tena," anasikika Ben-Gvir akijibu kupitia mkalimani.

"'Kunung'unika' magaidi kuhusu hali zilivyo katika magereza hakunishughulishi," ameandika pia waziri huyo wa kizayuni katika chapisho aliloambatanisha na video hiyo.

Mfungwa huyo wa kike alipoomba hali ya gereza iboreshwe, Ben-Gvir alikataa ombi lake.

Hii si mara ya kwanza kwa waziri huyo wa utawala wa kizayuni wa Israel kuingia kwenye seli za wafungwa wa Kipalestina kuwadhihaki na kuwakejeli.

Mapema mwezi Agosti, alimkejeli mfungwa mwanamke aliyelalamikia hali mbaya ya kizuizini alikowekwa na kukosekana mahitaji ya msingi, akimwambia "gereza si hoteli."

Tangu aliposhika wadhifa wa waziri wa usalama wa ndani wa utawala wa kizayuni mwishoni mwa 2022, Ben-Gvir amechukua hatua za kushadidisha mazingira mabaya ya kizuizini kwa wafungwa wa Kipalestina, ikiwa ni pamoja na kutekeleza sera za kuwashindisha na njaa na kutowapatia huduma za matibabu, pamoja na kuwahilikisha kwa mateso na kuwaweka kwenye seli za peke yao.

Kwa mujibu wa ripoti za mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Kipalestina na Israel, Wapalestina wanaokadiriwa kufikia 9,500 wanashikiliwa kwenye jela za utawala haramu wa Israel, wakiwemo wanawake 94 na zaidi ya watoto 350, ambao wanaatilika kwa njaa, mateso na kukosa kimatibabu…/