Wazayuni waendelea kuuvunjia heshima Msikiti wa al Aqsa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i1414-wazayuni_waendelea_kuuvunjia_heshima_msikiti_wa_al_aqsa
Walowezi wa Kizayuni na askari wa utawala ghasibu wa Israel wameendelea kuushambulia na kuuvunjia heshima Msikiti wa al Aqsa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 17, 2016 08:38 UTC
  • Wazayuni waendelea kuuvunjia heshima Msikiti wa al Aqsa

Walowezi wa Kizayuni na askari wa utawala ghasibu wa Israel wameendelea kuushambulia na kuuvunjia heshima Msikiti wa al Aqsa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Walowezi 47 wenye itikadi kali jana Jumanne walivuka mlango wa magharibi wa msikiti huo mtukufu ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu na kuingia ndani ya msikiti. Walowezi hao ambao walikuwa wakilindwa na kupewa himaya na makumi ya askari na polisi wa Israel, waliingia katika uwanja wa Msikiti wa al Aqsa na kuanza kurandaranda katika eneo hilo tukufu. Ripoti zinasema maafisa 50 wa vyombo vya upelelezi vya Israel pia walishiriki katika kitendo hicho cha kichochezi.

Wakati huo huo Wapalestina waliokuwa katika eneo hilo walikabiliana na wavamizi hao kwa kupiga takbira na kupambana nao. Wapalestina wanaoishi katika Ukingo wa Magharibi na Baitul Muqaddas walianzisha Intifadha ya Quds yapata miezi mitano iliyopita wakipinga vitendo viovu vya walowezi wa Kiyahudi vya kuuvunjia heshima Msikiti wa al Aqsa. Harakati hiyo ya Intifadha ya Wapalestina imeutia wasiwasi mkubwa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Waziri wa Usalama wa Ndani wa Israel, Gilad Erdan amekiri kwamba, utawla huo umeshindwa kuzima mapambano ya Intifadha ya Wapalestina na operesheni za wanamapambano hao na kusema askari polisi na jeshi la Israel wamepelekwa kwa wingi katika maeneo ya Ukingo wa Magharibi na Quds inayokaliwa kwa mabavu lakini hawajaweza kukabiliana na operesheni za Wapalestina.

Hivi karibuni pia mkuu wa chama cha mrengo wa kushoto cha Leba, Isaac Herzog alikiri kwamba, Israel imeshindwa kusimamisha Intifadha ya Quds na kuongeza kuwa Waziri Mkuu wa utawala huo, Benjamin Netanyahu ameshindwa kudhibiti hali ya mambo katika maeneo ya Ukingo wa Magharibi na Quds.

Kufuatia kushindwa kwa Israel kuzima mapambano na Intifadha ya Quds, hitilafu zimeshadidi zaidi kati ya jeshi la Israel na Idara ya Magereza ya utawala huo juu ya ongezeko kubwa la idadi ya wafungwa wa Kipalestina. Intifadha ya Quds ilianza Oktoba mwaka uliopita baada ya walowezi wa Kiyahudi kuuvunjia heshima Msikiti wa al Aqsa wakisaidiwa na jeshi la Israel. Imepita karibu miezi mitano sasa tangu kuanza harakati hiyo mpya ya mapambano ya Wapalestina na Israel inaendeleza siasa zake za kikatili na ukandamizaji. Takwimu zinaonesha kuwa, raia wasiopungua 170 wa Palestina wameuawa shahidi kwa kupigwa risasi katika mapambano hayo. Vilevile maelfu ya Wapalestina wamejeruhiwa na wengine wanashikiliwa katika korokoro za kutisha za utawala wa kigaidi wa Israel.