Palestina yaitaka dunia ikomeshe jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i14551-palestina_yaitaka_dunia_ikomeshe_jinai_za_utawala_wa_kizayuni_wa_israel
Mwakilishi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa ameutaka utawala wa Kizayuni wa Israel ukomeshe ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo uliyowapora Wapalestina.
(last modified 2026-05-13T18:57:29+00:00 )
Sep 03, 2016 11:43 UTC
  • Palestina yaitaka dunia ikomeshe jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel

Mwakilishi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa ameutaka utawala wa Kizayuni wa Israel ukomeshe ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo uliyowapora Wapalestina.

Shirika la habari la "Felestin Ma'an" limemnukuu Riyadh Mansour akitoa mwito huo na kuitaka jamii ya kimataifa ichukue maamuzi mazito ya kuulazimisha utawala wa Kizayuni ukomeshe jinai zake dhidi ya Wapalestina na iache kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina kama vile mashariki mwa mji wa Baytul Muqaddas.

Aidha mwakilishi huyo wa Palestina katika Umoja wa Mataifa amesema, jukumu la kuulazimisha utawala wa Kizayuni ukomeshe ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina, ni la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kusema kuwa, kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo waliyoporwa Wapalesstina ni uvunjaji wa wazi wa sheria za kimataifa.

Moja ya vitongoji vya walowezi wa Kizayuni vilivyojengwa katika ardhi walizoporwa Wapalestina

 

Aidha amewaandikia barua Ban Ki moon Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na mkuu wa Baraza la Usalama pamoja na mkuu wa Baraza Kuu la umoja huo na kuwakumbusha kuwa, zaidi ya miongo sita imepita sasa ambapo utawala wa Kizayuni unaendelea kufanya jinai dhidi ya Wapalestina na unaendelea kupora ardhi zao na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni, na hakuna hatua zozote za maana zilizochukuliwa.

Mwakilishi wa Palestina katika Umoja wa mataifa aidha amesema, ni jambo la wajibu kuundwa nchi huru ya Palestina katika mipaka ya mwaka 1967, mji mkuu wake ukiwa ni Baytul Muqaddas.