Marekani yasema mazungumzo baina yake na Russia kuhusu Syria yamevunjika
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imetangaza kuwa mazungumzo baina ya nchi hiyo na Russia kuhusu mgogoro wa Syria yamevunjika.
Afisa mmoja wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ametangaza leo kuwa pande hizo mbili zilikuwa zinakaribia mno kufikia mwafaka na kwamba Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo John Kerry na mwenzake wa Russia Sergei Lavrov walikuwa wanakaribia kukamilisha makubaliano hayo lakini saa kadhaa baadaye pande hizo mbili zilitangaza kuwa mazungumzo hayo yamevunjika.
Afisa huyo wa Washington ameongeza kuwa: "Warussia wamerejea kuzungumzia tena maeneo ambayo sisi tulidhani tumeshaafikiana; kwa hivyo tunarejea miji mikuu yetu kwa mashauriano zaidi".
Rais Barack Obama wa Marekani alinukuliwa hapo kabla pia akisema, bado hawajafikia hatua ya maafikiano juu ya usitishaji vita.
Obama ameashiria kulegalega kwa makubaliano ya huko nyuma ya usitishaji vita nchini Syria na kuongeza kuwa:"Tuna hitilafu kubwa za mitazamo sio tu kuhusiana na mirengo tunayoiunga mkono bali pia kuhusu mchakato utakaowezesha kurejesha amani nchini Syria".
Kwa mujibu wa afisa huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Kerry na Lavrov wanatazamiwa kukutana na kufanya mazungumzo tena kesho Jumatatu pembeni ya kikao cha viongozi wa nchi za kundi la G20 kinachofanyika mjini Hangzhou, China.
Taarifa ya kuvnjika mazungumzo baina ya Marekani na Russia kuhusu mgogoro wa Syria imetolewa katika hali ambayo mapema asubuhi ya leo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Ryabkov alikuwa ametangaza kuwa Washington na Moscow zilikuwa zinakaribia kufikia mwafaka.
Duru kadhaa za mazungumzo ya kimataifa yaliyofanyika hadi sasa kwa lengo la kuuhatimisha mgogoro wa Syria zimemalizika bila ya kupatikana tija.
Watu wanaokadiriwa kufikia 470,000 wameuawa kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja kutokana na vita na machafuko yanayoendelea kwa mwaka wa tano hivi sasa nchini Syria na wengine zaidi ya milioni moja na laki tisa wamejeruhiwa.../