Israel, chanzo cha kushadidi hali mbaya ya kiuchumi Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i15028-israel_chanzo_cha_kushadidi_hali_mbaya_ya_kiuchumi_palestina
Mashirika ya Kimataifa yameonya kuhusu kudorora kwa kiasi kikubwa uchumi wa ardhi za Palestina kutokana na vizingiti vilivyowekwa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Palestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 10, 2016 03:03 UTC
  • Israel, chanzo cha kushadidi hali mbaya ya kiuchumi Palestina

Mashirika ya Kimataifa yameonya kuhusu kudorora kwa kiasi kikubwa uchumi wa ardhi za Palestina kutokana na vizingiti vilivyowekwa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Palestina.

Taarifa ya Ijumaa ya Mfuko wa Kimataifa wa Fedha IMF  imesema hatua ya utawala wa Israel ya kuweka mzingiro katika Ukanda wa Ghaza na vizingiti vya kusafiri katika maeneo mengine ya Palestina katika kipindi cha miaka 10 sasa imepelekea kutostawi uchumi wa maeneo hayo na pia kusababisha kiwango cha ukosefu wa ajira kufikia asilimia 24 huku kukiwa na umasikini mkubwa katika maeneo hayo.

Siku ya Ijumaa pia Shirika la Ustawi na Biashara la Umoja wa Mataifa UNCTAD  limetoa taarifa ya kila mwaka na kubainisha wasiwasi wake kuhusu kuendelea mashinikizo ya Utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina. UNCTAD imesema hatua ya Israel ya kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina ni jambo ambalo limepelekea kuharibika uchumi wa Wapalestina.

Ripoti ya UNCTAD imesema Israel imepora au kuharibu ardhi za Palestina mbali na kuiba maji na nisharti ya Wapalestina. Aidha UNCTAD imebaini kuwa Israel inazuia kuuzwa bidhaa za Wapalestina, inauzingira Ukanda wa Ghaza huku ikiendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na wakati huo huo kuharibu masoko ya Wapalestina mambo ambayo yanafanya uchumi wa Palestina uwe tegemezi kwa Israel.

Nyumba za Wapalestina zilizoharibiwa na Israel huko Ghaza

Ripoti hizo mbili pia zimeashiria baadhi ya matitizo yanayotokana na mzingiro wa Ukanda wa Ghaza na kusema hali ya kiuchumi na kibinadamu ni mbaya mno kutokana Israel kuzuia ujenzi mpya wa eneo hilo baada ya vita.

Maafisa wa Wizara ya Uchumi wa Palestina wanasema kuwa yamkini ujenzi mpya wa Ghaza ukachukua makumi ya miaka kutokana na hatua ya Utawala wa Kizayuni wa Israel kuzuia vifaa vya ujenzi kuingia eneo hilo na pia kutokana na  nchi tofauti kuvunja ahadi zilizotoa kuhusu ukarabati mpya wa Ghaza. Itakumbukwa kuwa eneo la Ukanda wa Ghaza lilikabiliwa na hujuma ya kinyama ya utawala wa Kizayuni wa Israel mwaka 2014 ambapo kulikuwa na uharibifu mkubwa mbali na kuuawa shahidi watu zaidi ya 2,000 wakiwemo watoto 500. Eneo hilo lilipata hasara ya mabilioni ya dola kutokana na hujuma hiyo ya Israel iliyolenga miundombinu na nyumba za raia.

Hivi karibuni Benki ya Dunia iliwasilisha ripoti ikiashiria hali mbaya katika ardhi za Palestina hasa Ukanda wa Ghaza baada ya hujuma ya Israel Juni 2014. Benki hiyo imezitaka serikali za Qatar, Imarati, Saudi Arabia na serikali zingine za Kiarabu katika Ghuba ya Uajemi kutekeleza ahadi zao za kukarabati upya Ukanda wa Ghaza.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni za Benki ya Dunia, eneo la Ghaza limepata sehemu ndogo tu ya ahadi za  dola bilioni nne zilioahidiwa na jamii ya kimataifa hasa nchi za Kiarabu. Kutokana na kutotekelezwa ahadi hizo, hivi sasa eneo la Ghaza linakabiliwa na matatizo mengi hasa katika sekta ya nyumba za makazi na miundombinu.

Nyumba za Wapalestina zilizoharibiwa na Israel huko Ghaza

Katika hali kama hii, wakuu wa Palestina wanasisitiza kuwa lazima mzingiro na vizingiti vyote vya Israel Palestina viondolewe. Iwapo jamii ya kimataifa haitachukua hatua za kuushurutisha utawala wa Kizayuni wa Israel kusitisha  mzingiro katika ardhi za Palestina, katika siku za usoni si tu kuwa matatizo ya Wapalestina yatashadidi bali pia kutajiri maafa ya kibinadamu katika eneo hilo.