HAMAS: Intifadha ya Quds itaendelea
(last modified Tue, 13 Sep 2016 04:15:10 GMT )
Sep 13, 2016 04:15 UTC
  • HAMAS: Intifadha ya Quds itaendelea

Kiongozi mwandamizi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesema kuna ulazima wa kuendelezwa Intifadha ya Quds dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Khalil al-Hayyah, kiongozi mwandamizi wa Hamas na Khatibu wa Sala ya Idi katika Ukanda wa Gaza amesema, madamu ukaliaji wa mabavu wa ardhi za Palestina na jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Palestina zinaendelea, Intifadha ya Quds dhidi ya utawala huo ghasibu nayo pia itaendelezwa. 

Mbali na kutilia mkazo umoja baina ya Wapalestina kwa ajili ya kukabiliana na ukaliaji wa mabavu wa ardhi za Palestina unaofanywa na utawala haramu wa Israel, Al-Hayyah ameongeza kuwa Intifadha ni njia ya kufikia umoja huo na kuhitimisha ukaliaji huo wa mabavu. 

Ufukwe wa Magharibi ndio kitovu cha Intifadha ya Quds

Tangu mwezi Oktoba mwaka uliopita wa 2015 maeneo mbalimbali ya Palestina yamekuwa yakishuhudia maandamano makubwa ya Wapalestina ya kupinga sera za kivamizi za utawala wa Kizayuni na njama za utawala huo haramu za kutaka kupotosha utambulisho wa mji wa Baitul Muqaddas na kuugawa Msikiti mtukufu wa Al-Aqsa kieneo na kinyakati baina ya Wazayuni na Wapalestina.

Hatua hizo za kichokozi na jinai za utawala haramu wa Israel zimekuwa cheche ya kuanza Intifadha ya Quds. 

Hadi sasa zaidi ya Wapalestina 230 wameuawa shahidi kwa kupigwa risasi na askari wa utawala wa Kizayuni na wengine wengi wamejeruhiwa.../

Tags