Mamlaka ya Ndani ya Palestina yalaumiwa kwa kushirikiana kiusalama na Israel
Kiongozi mmoja wa Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina amesema harakati hiyo imesikitishwa na hatua ya Mamlaka ya Ndani ya kushirikiana kiusalama na utawala wa Kizayuni wa Israel huku utawala huo haramu ukiendelea kuwaua Wapalestina.
Khadhr Adnan, ameliambia gazeti la Palestina la Al-Risalah kuwa Mamlaka ya Ndani ya Palestina inayoongozwa na Mahmoud Abbas ina maelfu ya silaha lakini haizitumii silaha hizo kukabiliana na Wazayuni maghasibu na kuongeza kuwa hatua ya mamlaka hiyo ya kushirikiana na utawala huo haramu wakati mauaji na ukandamizaji wa Tel Aviv dhidi ya Wapalestina ungali unaendelea haiwezi kukubalika.
Huku akiashiria kwamba Mamlaka ya Ndani ya Palestina haijasita kuchukua kila hatua kuikandamiza Intifadha ya Quds, Adnan amesema hatua hizo zinachukuliwa katika hali ambayo jinai za Wazayuni dhidi ya Wapalestina na ususiaji kula wa Wapalestina wanaoshikiliwa kwenye magereza ya Israel wakiwemo ndugu wawili wa familia ya Al-Balbul na Malik al-Qadhi ungali unaendelea.
Kiongozi huyo mwandamizi wa harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina aidha amesema kutiwa nguvuni wanaharakati wa Kipalestina na viongozi wa muqawama katika Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan kwa lengo la kusimamisha vuguvugu la Intifadha ni doa jeusi katika historia ya Palestina na akabainisha kuwa licha ya hatua ya Mamlaka ya Ndani ya kutumikia maslahi ya Wazayuni muqawama wa heshima na sharafu wa Palestina chini ya kivuli cha kushamirisha Intifadha ya Quds itaendelea.
Wakati huohuo askari wa utawala wa Kizayuni wamewaua shahidi kwa kuwapiga risasi vijanawawili wa Kipalestina katika Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan. Kwa kuuawa vijana hao, idadi ya Wapalestina waliouliwa shahidi tangu ilipoanza Intifadha ya Quds mwezi Oktoba 2015 imefikia 247.../