Russia: Hatuna matumaini ya kufanikiwa mazungumzo ya Lausanne
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i17422-russia_hatuna_matumaini_ya_kufanikiwa_mazungumzo_ya_lausanne
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ametabiri kuwa mazungumzo yatakayofanyika leo (Jumamosi) katika mji wa Lausanne nchini Uswisi kuhusu Syria hayatakuwa na natija ya maana.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 15, 2016 00:27 UTC
  • Russia: Hatuna matumaini ya kufanikiwa mazungumzo ya Lausanne

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ametabiri kuwa mazungumzo yatakayofanyika leo (Jumamosi) katika mji wa Lausanne nchini Uswisi kuhusu Syria hayatakuwa na natija ya maana.

Sergei Lavrov amegusia mazungumzo ya kusaka amani ya Syria huko Lausanne Uswisi na kueleza kuwa Moscow haina matumaini na mazungumzo hayo na inadhani kuwa hakuna matunda yoyote ya maana yatakayopatikana. Amesema hii ni kwa sababu hadi kufikia sasa nchi washirika wa Magharibi hazijachukua hatua yoyote inayokubalika ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Syria.

Eneo moja la Syria lilivyogeuka na kuwa magofu baada ya kuathiriwa na vita na machafuko

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameongeza kusema kuwa, msimamo wa Moscow katika mazungumzo hayo utakuwa wa kweli kikamilifu na kwamba Russia haina nia ya kuwasilisha mpango mpya katika mazungumzo hayo kuhusu Syria.  Sergei Lavrov amesema, Moscow itaendelea kufuatilia hatua zinazoeleweka ambazo ni za dharura kwa ajili ya utekelezaji wa maazimio ya Baraza la Usalama  huko Lausanne; ikiwa ni pamoja na kuhimiza kutekelezwa makubaliano yaliyofikiwa kati ya Marekani na Russia kuhusiana na Syria.

Mazungumzo ya amani ya Syria yanafanyika leo Jumamosi katika mji wa Lausanne nchini Uswisi kwa kuhudhuriwa na wawakilishi wa Marekani, Russia na nchi kadhaa muhimu za eneo hili.