Ansarullah: Umoja wa Mataifa uchunguze ukatili wa Saudia Yemen
Harakati ya Ansarullah ya Yemen imetoa wito wa kufanyika uchunguzi wa kimataifa juu ya mauaji ya kinyama yaliyofanywa na ndege za kivita za Saudi Arabia nchini Yemen hivi karibuni.
Harakati hiyo ya Houthi imemtaka Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kubuni jopo huru la uchunguzi litakalowajumuisha shakhshia wa kimataifa wenye misimamo ya wastani kufanya uchunguzi huo.
Haya yanajiri siku chache baada ya Saudi Arabia kukiri kuwa ndiyo iliyofanya mashambulizi katika ukumbi ambao ulikuwa umekusanyika mamia ya watu kwa ajili ya mazishi kusini mwa Sana'a, mji mkuu wa Yemen.
Katika mashambulizi hayo ya tarehe 8 mwezi huu wa Oktoba, watu zaidi ya 160 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa. Hayo yalikuwa ni mauaji makubwa zaidi kuwahi kufanywa na Saudi Arabia tangu ilipoanzisha uvamizi wake mwezi Machi 2015 huko Yemen.
Mashirika 99 ya haki za binadamu ya Kiarabu yametoa taarifa yao na kueleza kuwa, jinai za kutisha na maafa yaliyofanywa na ndege za kijeshi za Saudia kusini mwa mji mkuu wa Yemen, Sana'a, Jumamosi jioni, ni mfano wa wazi kabisa wa jinai za kivita dhidi ya binadamu.
Ukatili huo unaendelea kulaaniwa hadi leo hii kote ulimwenguni huku shirika la Human Rights Watch likisema kuwa hiyo ni jinai ya wazi ya kivita.