Maafisa wawili wa usalama wa Saudia wauawa mjini Dammam
Watu wasiojulikana wamewapiga risasi na kuwaua maafisa wawili wa usalama katika mji wa Dammam mashariki mwa Saudi Arabia.
Taarifa zinasema washambuliaji hao waliwafyatulia risasi maafisa hao wa usalama leo Jumanne wakati wakitoka kazini wakiwa ndani ya gari binafsi.
Saudi Arabia imekuwa ikishuhudia visa vya ufyatuaji risasi na mashambulizi ya mabomu tokea vikosi vya usalama vianze kuwalenga Waislamu wa madhehebu ya Shia katika kipindi cha mwaka mmoja sasa.
Mwezi Septemba, maafisa wawili wa polisi walipigwa risasi na kuuawa Dammam, mji mkuu wa mkoa wa Mashariki ambao wakaazi wake wengi ni Waislamu wa madhehebu ya Shia wanaokandamizwa na utawala wa Saudia. Aidha kumekuwepo na hujuma kadhaa dhidi ya misikiti ya Waislamu wa madhehebu ya Shia katika eneo hilo.
Serikali ya Saudia inalaumu magaidi wa kitakfiri wa ISIS au Daesh kuwa ndio wanaotekeleza hujuma hizo. Ikumbukwe kuwa magaidi wa ISIS wanafuata itikadi ya Kiwahabi ambayo ni itikadi rasmi ya Saudi Arabia.